MAUZA UZA PAKA WA AJABU ATIKISA NYUMBANI KWA MSANII

UKISIKIA neno mauzauza maana yake ni hali ya ovyoovyo isiyotambulikana; hii ndiyo imedaiwa kuletwa na paka wa ajabu nyumbani kwa msanii wa Bongo Muvi, Jully Tax.  Kumtambua Jully Tax ambaye kwa sasa maskani yake ni Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, ni yule aliyeigiza muvi ya Saradini ambapo baada ya kupotea kwenye sanaa ameibuka na madai ya nyumba yake kutikiswa na mambo aliyoyaita ya kichawi.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko hivi karibuni msanii huyo alisema: “Kabla ya huyu paka kuja kufa mlangoni kwangu siku mbili zilizopita kuna panya mwenye ukubwa wa  kushangaza alifia ndani. “Naona mambo haya si ya kawaida katika maisha yangu, nimewaita mshuhudie huyu paka na mkawaambie mashabiki wangu kuwa nikifa; wajue kuna mtu ameniua,” alisema masanii huyo katika mazungumzo yake na waandishi wetu.

KWA NINI AHISI KUROGWA?

Waandishi wetu walipomuuliza kwa nini anahusisha tukio la wanyama hao kufia kwake na masuala ya kishirikina msanii huyo alimtaja mama mmoja (jina linahifadhiwa) kuwa alimwambia kuwa atamroga na kwamba matukio hayo ni kama ishara kwake kuwa alichoambiwa kinaenda kutimia.

Kwa kuwa gazeti hili haliamini masuala ya kishirikina linaona hakuna busara kuuhusisha ugomvi wa msanii huyo na mwanamke mmoja na mambo hayo ya paka na panya kufia nyumbani kwa Jully Tax.

MATUKIO YA KUSHANGAZA

Hata hivyo; kwa kuwa waandishi wetu waliungana na baadhi ya majirani, walishuhudia mambo yaliyofikirisha kutoka kwa mzoga wa paka huyo aliyedaiwa kufa usiku baada ya kutoa povu puani na baadaye kuanza kutokwa na damu puani.

Matukio hayo mawili yalipishana muda kama wa dakika kumi toka watu wakusanyike nyumbani kwa msanii huyo na kuwafanya wengi wapigwe na butwaa. “Ona alikuwa anatoka puvu lakini sasa anavuja damu au hajafa jamani?” alihoji mmoja kati ya majirani na kumfanya mwingine auchunguze mzoga wa paka huyo na kubaini umeshatoka uhai muda mrefu.

MAMA APAGAWA MAPEPO

Katika hali nyingine ya kushangaza; mama mmoja aliyekuwepo eneo la tukio hilo ghafla alianza kupiga kelele na kudaiwa kuwa amepagawa na mapepo na kuanza kutamka maneno yaliyojaa utata.

“Utakufa, umeambiwa uhame hapa lakini husikii, shauri yako,” alisema mwanamke huyo akimaanisha kumuonya Jully Tax. Kwa nini ahame kwenye nyumba hiyo na atakufaje?; ni mambo ambayo tumeamua kutoyapa kipaumbele katika habari hii kwa sababu taja hapo huu.

USTADHI AITWA

Wakati hayo yakiendelea nyumbani kwa msanii huyo mara kijana aliyekuwa amevaa kanzu na kutambulishwa kama ustadhi wa dini ya Kiislamu aliwasili na kuanza kushuka dua.

Aidha, mara baada ya kumalizika kwa dua hiyo hali ya mambo ilitulia ingawa Jully Tax aliendelea kuwa na wasiwasi juu ya kile alichokiita, ‘roho yake kutafutwa’ iuawe kichawi. Hata hivyo, ustadhi alimwambia msanii huyo kuwa aendelee kuamini katika Mungu na kwamba ndiye kinga ya mwanadamu kwa jambo lolote baya.


Loading...

Toa comment