The House of Favourite Newspapers

Mauzo ya Hisa ya DSE Yapaa, Yafikia Trilioni 20.3

0
Patrick Msusa Meneja Masoko wa Soko la Hisa La Dar es Salaam.

MAUZO ya hati fungani katika  Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wiki iliyoishia tarehe Aprili 13, 2017 yamepaa kutoka thamani ya Shilingi Trilioni 20 wiki iliyopita hadi Shilingi Trilioni 20.3. ikitokana na kuongezeka kwa bei za hisa za  Acacia kwa asilimia 7%, Jubilee Holdings 6.7% na DSE 3.3%.

Hiyo ni baada ya mauzo ya hati fungani tatu za serikali zenye jumla ya thamani ya Shilingi Bilioni 8.8 kwa jumla ya gharama ya Shilingi Bilioni 6.9.

Hayo yamesemwa na Meneja Masoko na Mauzo DSE, Patrick Msusa, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, ambapo amesema pia Idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa imepungua kutoka hisa 1,700,000 hadi hisa 465,000 zenye thamani ya mauzo ya Shilingi Bilioni 1.7 kutoka Shilingi Bilioni 13.9 wiki iliyopita.

Hata hivyo, amesema ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko  umeongezeka kutoka Sh. Trilioni 20 wiki iliyopita hadi Trilioni 20.3 wiki iliyoishia tarehe 13 Aprili 2017 baada ya kuongezeka kwa bei za hisa za Acacia kwa asilimia 7%, Jubilee Holdings 6.7% na DSE 3.3%.

Wakati huohuo, mtaji wa kampuni za ndani umeendelea kubaki kwenye kiwango cha awali cha Shilingi Trilioni 7.5 wiki hii.

“Kiashiria cha kampuni zilizoorodheshwa katika soko  kimeongezeka kwa pointi 39 kutoka pointi 2,297 hadi pointi 2,336 kutokana na kuongezeka kwa bei za hisa za kampuni mbalimbali zilizopo sokoni.

Kiashiria cha kampuni za ndani yaani TSI kimeendelea kubaki kwenye wastani wa pointi 3,573 wiki hadi wiki,” amesema.

“Sekta ya viwanda (IA) wiki hii imeendelea kubaki kwenye kiwango cha awali cha pointi 4,618. Sekta ya huduma za kibenki na kifedha (BI) wiki hii imepanda kwa pointi 1 kutoka pointi 2,546 hadi pointi 2,547. Huku sekta ya huduma za kibiashara (CS) wiki hii imebaki kwenye kiwango cha awali cha pointi 3,137.”

Aidha, ametaja Kampuni zilizoongoza katika mauzo ya hisa kuwa ni TBL kwa      92.3%, CRDB2.86% na NMB   2.1%.

Leave A Reply