The House of Favourite Newspapers

Mayanja ndiye bosi Simba Sc

0

Hans Mloli na Nicodemus Jonas
MECHI tatu, ameshinda zote, hajafungwa bao lolote. Huyu ni Jackson Mayanja ambaye alisaini Simba kama kocha msaidizi lakini taarifa zimesema uongozi wa klabu hiyo umeamua awe kocha mkuu hadi mwisho wa msimu.
Mayanja amepewa mikoba hiyo kutokana na mazungumzo kati ya Simba na kocha Mdenishi, Kim Poulsen kukwamia kwenye suala la maslahi na dili la Hemed Morocco nalo kufa dakika za mwisho, baada ya kuahidiwa atalipwa mshahara wa Sh milioni tano, lakini alipotua Dar wakageuka, wakaziona nyingi na wakamuwekea mezani Sh milioni nne, akachomoa, akabeba mabegi yake na kurudi zake Zenji.
Pia taarifa zinasema uongozi wa Simba unaridhishwa na mwenendo wa timu hiyo kwa sasa ikiwa chini ya Mganda huyo ambaye ameonyesha mabadiliko makubwa kiasi cha kumfunika Muingereza, Dylan Kerr.
Mchezo wa kwanza kwa Mayanja ulikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar ambao alishinda bao 1-0, kisha akashinda 2-0 dhidi ya JKT Ruvu kabla ya juzi Jumamosi kushinda mabao 3-0 dhidi ya Burkina Faso kwenye Kombe la FA ugenini.
Mratibu wa Simba, Abass Ally, amesema: “Kikubwa ambacho mpaka sasa unaweza kumzungumzia Mayanja, amefanikiwa kutatua tatizo la fitness na ndiyo maana timu inaonekana kuanza kucheza soka dakika 90, tofauti na ilivyokuwa kwa Kerr. Awali ilikuwa haiwezi kufika dakika 90, lakini angalau kwa sasa unaona timu inapambana na inacheza soka linaeleweka muda wote.”
Kwa upande wa Mganda huyo alisema mfumo wake ni soka la kusaka mabao na siyo kupaka rangi mipira pamoja na kuhakikisha wachezaji wanacheza wakiwa na pumzi ya kutosha muda wote.
“Kwa kipindi hiki, najaribu kuwarudisha wachezaji kwenye utimamu wa kucheza dakika zote. Napenda kuona soka la kusaka magoli na timu kupigana mwanzo-mwisho, hiyo ndiyo falsafa yangu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Coastal Union, Kiyovu ya Rwanda na timu ya taifa ya Uganda.
Mtu wa ndani kutoka Simba amelijuza Championi Jumatatu kuwa, masharti ya Kim kwenye suala la pesa ni magumu kulingana na hali mbaya ya pesa iliyopo Simba kwa sasa, lakini wana mpango wa kumkabidhi timu kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars, mara baada ya kumalizika kwa msimu huu.
Kutokana na hilo, upande wa pili wa shilingi sekretarieti ya timu hiyo imekubaliana kumpa timu Mayanja mpaka mwisho wa msimu huku akitafutiwa msaidizi makini.
Katika kuanza mchakato huo wa kutafuta msaidizi, jina la kwanza likawa la Juma Mgunda ambaye mara ya mwisho alikuwa ni kocha msaidizi wa timu ya Kilimanjaro Stars chini ya kocha mkuu Abdallah Kibadeni.
Lakini jina hilo lilionekana kupingwa na viongozi wengi kwa sababu tofautitofauti zikiwemo za kiutendaji na sasa mchakato bado unaendelea kuangalia nani anaweza kuchukua nafasi hiyo na akawa mwenye mchango mkubwa kwa ajili ya kuhakikisha Simba inamaliza ligi katika mazingira mazuri msimu huu.
“Bado tunaendelea kucheki nani anaweza kuchukua hii nafasi maana tumejaribu kwa Mgunda, wengi wamepinga, kwa hiyo tupo kwenye mchakato huo.
“Kim tumezungumza naye lakini yupo juu sana katika dau halafu na masharti yake ya kutaka kuishi Masaki nayo yamekuwa magumu kidogo, uzuri ni kwamba tumemwambia atachukua timu msimu ujao kwa hiyo bado mazungumzo yanaendelea,” kilisema chanzo.
Mayanja alipoulizwa kuhusiana na taarifa za kuwa kocha mkuu, alisema hajui chochote lakini Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema suala hilo litapatiwa ufafanuzi baadaye.
“Vuteni subira, suala hilo halijafika muda wake. Tutalitolea ufafanuzi muda ukifika,” alisema Kaburu.

Leave A Reply