Mayele Aitikisa Afrika Ofa nne Zatua Mezani mwa Yanga
JUMLA ya ofa nne zipo mezani mwa Yanga, kutoka klabu tatu kubwa Afrika zikimuhitaji mshambuliaji wa timu hiyo, Mkongomani Fiston Mayele katika msimu ujao.
Mkongomani huyo hivi sasa gumzo Afrika kutokana na kiwango bora ambacho amekionyesha katika Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Mshambuliaji huyo ni kinara wa mabao katika Kombe la Shirikisho Afrika akifunga mabao sita akiwa sawa na straika wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Ranga Chivaviro.
Taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, ni kuwa klabu ya US Berkane, Raja Casablanca zote za nchini Morocco na Orlando Pirates ya Afrika Kusini ndio zipo katika vita za kuwania saini ya mshambuliaji huyo.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa ofa hizo zote zilizoletwa Yanga zina ushawishi kutokana na dau la usajili walilotajiwa ambalo ni siri kwa sasa hivi.
Aliongeza kuwa uongozi wa timu hiyo, umepanga kufanya kikao mwishoni mwa msimu huu kwa ajili ya kupitia ofa hizo ambazo kama wakivutiwa nazo, basi watamuachia nyota huyo.
“Mpaka sasa uongozi wetu umepokea ofa zaidi ya tatu kubwa kutoka klabu mbalimbali hasa za Afrika Kusini na Morroco ambazo zote zinataka kutushawishi tukubali kumuachia Mayele.
“Klabu hizo zote zinamtaka kwa ajili ya msimu ujao, hivyo uongozi umepanga kukaa kufanya kikao mwishoni mwa msimu kwa ajili ya kujadili ofa hizo kuona ipi yenye ushawishi na kama watakosa basi Mayele ataendelea kubakia.
“Lakini upo uwezekano mkubwa wa uongozi kugomea mipango hiyo ya kumuachia Mayele, kwani bado anahitajika kuwepo hapo kwa ajili ya michuano ya kimataifa msimu ujao,” alisema mtoa taarifa huyo.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said hivi karibuni alizungumzia mipango ya usajili kwa kusema: “Kama uongozi tuna mipango ya kuisuka timu itakayokuwa imara na tishio Afrika. Hivyo hatutakuwa tayari kumuachia mchezaji yeyote kuondoka ambaye yupo katika mipango ya kocha wetu Nabi (Nasreddine), zipo ofa kadhaa za wachezaji wetu kuhitajika na klabu.”
Kutokana na uwezo wa juu ambao ameuonyesha Mayele kwa msimu huu thamani yake inatajwa kufikia zaidi ya bilioni 2 ambapo fedha hizo Yanga wamepanga kusajili mastraika wengine ambapo kwa sasa wanahusishwa na straika Ranga Chivaviro wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
STORI NA WILBERT MOLANDI
SINGIDA BIG STARS vs YANGA: KAULI ya KOCHA KAZE, AFUNGUKA MAANDALIZI – ”UTAKUWA MGUMU”…