Kartra

Mayele: Nakuja Yanga Jumapili

TWENDENI tukawapokee! Ndio kauli inayoweza kutumika kwa sasa mara baada ya mchezaji wa kimataifa wa DR Congo, Fiston Mayele kuthibitisha kuwa atatua nchini keshokutwa Jumapili.

 

Wakati huohuo, beki wa kulia, Shabani Djuma, amekiri kuwa yeye atachelewa kutua nchini ambapo atatua Agosti 4 akitokea nchini DR Congo.

Yanga imekamilisha usajili wa wachezaji hao ambao wote walikuwa wakicheza katika Klabu ya AS Vita ambapo Djuma tayari ameshasaini mkataba wa miaka 2 huku Fiston Mayele akitarajiwa kusaini makataba pindi atakapotua nchini.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mayele alisema anatarajia kutoka DR Congo siku ya Jumamosi Julai 31 na kufika nchini Agosti 1 ambayo itakuwa Jumapili.“Natarajia kuondoka nchini DR Congo siku ya Jumamosi kisha kufika Tanzania siku ya Jumapili ambayo itakuwa Agosti 1, sitakuja na Shabani Djuma kama ambavyo ilitakiwa iwe hivyo hapo awali.

 

“Mimi nitakuwa tofauti na Djuma kwani nikifika Tanzania  nitasaini mkataba kisha nitarejea tena nyumbani DR Congo na baadaye nitarudi tena tayari kwa kujiunga moja kwa moja na Yanga,” alisema mshambuliaji huyo.

 

Kwa upande wa Djuma yeye alisema: “Natarajia Agosti 4 kufika Tanzania tayari kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, nitakuja moja kwa moja ambapo kila kitu kuhusu maisha mapya nikiwa huko nimehakikishiwa na uongozi wa Yanga.”

STORI: MARCO MZUMBE, Dar es Salaam


Toa comment