LICHA ya kufanikiwa kufunga mabao saba katika michezo mitatu iliyopita ya ligi, staa wa Yanga, Fiston Mayele amesema kuwa bado kazi hajamaliza kwani atahakikisha anafunga mabao mengi kutokana na nafasi atakazokuwa anazipata.
Mayele amefanikiwa kufunga mabao saba katika michezo mitatu mfululizo ambapo alifunga matatu dhidi ya Singida Big Stars, mawili dhidi ya Dodoma Jiji na mabao mawili dhidi Mbeya City na kufikisha mabao 10 akiwa ndiyo kinara wa utupiaji.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mayele alisema kuwa licha ya kufunga idadi hiyo ya mabao lakini kwake bado ataendelea kupambana kuhakikisha anafunga ili aweze kuisaidia Yanga kufanya vyema katika michezo yote iliyosalia na kutwaa ubingwa.
“Nafahamu kuwa ni idadi kubwa ya mabao, mabao saba katika michezo mitatu ni namba nzuri ukiwa kama mshambuliaji, kwa upande wangu namshukuru Mungu kuona nazidi kuifungia Yanga mabao mengi na muhimu zaidi.
“Kikubwa ni mimi kuona naendelea kuzitumia nafasi za mabao ambazo nitazipata naamini kila kitu kitakuwa sawa, mashabiki, viongozi, benchi la ufundi na hata sisi wachezaji tunatamani kuona kila mara tunapata matokeo mazuri na mwisho wa msimu tuweze kuwa mabingwa,” alisema mchezaji huyo.
Stori: Marco Mzumbe