The House of Favourite Newspapers

Mazishi ya MARIA na CONSOLATA; Iringa yazizima, ni vilio kila kona

IRINGA: PACHA walioungana Maria na Consolata Mwakikuti waliofariki dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya Rufaa Iringa, wameifanya Iringa nzima kuzizima kwa huzuni wakati shughuli za mazishi zikiendelea.

Pacha hao walitarajiwa kuzikwa jana kwenye mji mdogo wa Tosamaganga, Iringa.

Watu wengi waliohudhuria msiba huo tangu Juni 2, mwaka huu mjini Iringa, walionekana kujawa majonzi huku kila mmoja akitamani kuwasindikiza wapendwa hao katika makazi yao ya milele.

Misa ya kuwaombea marehemu hao ilitarajiwa kuongozwa na Askofu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa na Askofu Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, shughuli ya kuaga mwili wa pacha hao, zilitarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu).

Mkuu wa Shirika la Maria Consolata, Sista Jane Nugi alisema, uamuzi wa kuwazika hapo umetokana na matakwa yao ambapo enzi za uhai wao walichagua kuzikwa kwenye eneo hilo, wanalozikwa viongozi wa madhehebu ya Katoliki.

“Wakati wakiumwa walisema wangetamani kuhifadhiwa tutakapohifadhiwa sisi, ndio maana tumepanga kuwazika katika Makaburi ya Tosamaganga,” alisema Sista Jane. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema pacha hao watazikwa kwenye jeneza moja ambalo lina mfumo wa watu wawili.

Daktari bingwa wa upasuaji na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Iringa, Dk. Mseleto Nyakiloto alizungumzia jinsi vifo vyao vilivyotokea kwa kufuatana.

“Mmoja alitangulia na mwingine alifariki baada ya dakika kumi, Maria ndio alikuwa ana tatizo la kiafya kwa kuwa mapafu yake yalishindwa kufanya kazi na huyu mwingine alikufa kutokana na viungo vingi katika mwili wao wanavitumia kwa pamoja,” Dk. Nyakiloto aeleza.

Hata hivyo, daktari huyo aliongeza kwa kusema kwamba mzunguko wa hewa na damu ndio umesababisha kifo cha mwingine hivyo matarajio ya mmoja kupona yasingewezekana.

Aidha, Dk. Nyakiloto alisema pacha wa aina hii wapo wa aina nyingi ingawa muda wa maisha yao huwa unatofautina kutokana mazingira pia; kuna wale ambao hawafikii hatua ya kuzaliwa, wengine wanakaa muda mfupi wanafariki na wengine hufikia umri mkubwa kama wa kina Maria na Consolata ambao wameweza kufikisha miaka 22.

Stori: Mwandishi Wetu, Amani

Comments are closed.