KIBAHA: Wakati tukio la mume, Hussein Zaid (58) na mke wake mdogo, Zainabu Juma (42) wakazi wa Mtaa wa Kilimahewa, Kata ya Mailimoja, Kibaha mkoani Pwani kufariki dunia kwa kujilipua kwa moto likiwa bado halijapoa, jipya limeibuka wakati wa mazishi ya wawili hao.
Wanahabari wetu ambao walikuwepo kwenye mazishi hayo wakianzia kwenye msiba wa mwanamke ambapo shughuli za mazishi zilifanyika kwenye nyumba ya mwanamke huyo iliyopo Kijiji cha Kilimahewa Kibaha, eneo ambalo tukio lilitokea.
Wanahabari wetu wakiwa msibani hapo walifanikiwa kuzungumza na wakazi wa eneo hilo kujua chanzo cha tukio hilo ambapo mmoja wa majirani wa eneo hilo ambaye alisema naye alihusika katika zoezi la kuvunja mlango wakati Zainab akipiga kelele alisema:
“Mimi huyo Zainab ni jirani yangu wa miaka mingi hapa mtaani ambapo kabla ya kuishi na Hussein ambaye tumemzoea kwa jina la Ustaadh, alishaishi na wanaume wengine kama watatu, huyu Ustaadh ni wanne. “Wanaume wote hao hakuweza kudumu nao muda mrefu lakini huyu ndiyo walionekana kupendana sana na hakuna ambaye alikuwa hajui hilo hapa mtaani.
“Sasa unajua ndugu mwandishi mapenzi yakizidi sana nayo huwa ni shida maana walikuwa wakioneana sana wivu hali iliyosababisha hivi karibuni mume kumshikia kisu mkewe na kutaka kumchoma lakini mwanamke alifanikiwa kujiokoa na kumuomba radhi mumewe yakaisha,” alisema jirani huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Aliendelea kudai jirani huyo kuwa, anavyofahamu historia ya penzi la wawili hao lilianza kunoga wakati Ustaadh mambo yake yakiwa supa ambapo alimuacha mkewe (Mkubwa) Evelina Sospeter na kuhamishia penzi kwa Zainab ambaye ni maarufu kama Cheupe Dawa.
Aliendelea kusimualia jirani huyo kuwa, mapenzi yakiwa yamenoga na jamaa akiwa na pesa za kutosha alimfanyia mambo mbalimbali Cheupe Dawa ikiwemo kumkarabatia nyumba yake.
VYUMA BAADA YA KUKAZA
Baada ya Ustaadh kuwekeza vya kutosha kwa Cheupe Dawa, hali ya kimaisha ilianza kumuwia ngumu kama wasemavyo vyuma kukaza ndipo jamaa akaanza kuhisi anaibiwa kwa kuwa hana kitu na hapo ndipo ilipoanza mizozo ya mara kwa mara.
Jirani huyo alidai kuwa baada ya jamaa kuishiwa Cheupe Dawa ni kama alikuwa akimfanyia visa Ustaadh aondoke amuache asonge na maisha yake ndipo jamaa akaona hawezi kurudi kwa mkewe aliyemuacha akiwa na fedha ni bora ajilipue na Cheupe Dawa ili wote wakose.
Waandishi wetu walizungumza na mama mzazi wa Zainab aliyejitambulisha kwa jina la Bitiali Hassan na kumhoji kufuatia tukio la kifo cha mwanaye ambapo alianza kusema;
“Mimi nilikuja hapa Kibaha nikitokea Chalinze ambapo napo nilikuja mwezi uliopita kutoka mkoani Kilimanjaro kuja kwenye msiba wa mwanangu mwingine uliokuwa hapo Chalinze.
“Hivi tunavyoongea leo ilikuwa ndiyo arobaini ya huyo marehemu lakini ndiyo yanatokea haya majanga, nampoteza mtoto mwingine ndani ya siku chache, ukweli inaniuma sana.” Akizungumzia suala la migogoro ya mwanaye huyo na mumewe enzi la uhai wao alisema hakuwahi kusikia migogoro yoyote katika maisha yao zaidi ya mzozo aliousikia siku ya tukio.
Awali, ilielezwa kuwa vifo hivyo vilitokea baada ya Zaid kumtuhumu mke wake kukosa uaminifu ndani ya ndoa, hali iliyomlazimu kufanya jaribio la kutaka kumchoma kwa kisu, ambalo halikufanikiwa kabla ya kuamua kukusanya nguo zote kisha kuziwasha kwa kutumia kiberiti.
Baada moto kushika kasi, wananchi wakisaidiana na polisi walifanikiwa kuwaokoa watu hao, hatimaye kuwakimbiza Hospitali ya Teule ya Tumbi kwa ajili ya matibabu.
Juhudi za madaktari Hospitali ya Tumbi ziliposhindikana wakawakimbiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi ambapo hata hivyo hawakuweza kuokoa uhai wa wawili hao. Mwanaume alifariki Juni 25, mwanamke Juni 26.
STORI: Richard Bukos na Neema Adrian, Risasi Jumamosi
Comments are closed.