Mazishi ya Rais Moi, Barabara Zafungwa Nairobi

MALORI na magari mengine ya mazigo hayaruhusiwi kutumia barabara kuu ya Nairobi – Eldoret huku maelfu ya waombolezaji wakitumia barabara hiyo yenye shughuli nyingi kuhudhuria mazishi ya rais mstaafu hayati Daniel Moi eneo la Kabarak Kaunti ya Nakuru.

 

Maafisa wa polisi wamepangwa katika barabara kuu kutoka Nairobi hadi Kabarak kuhakikisha kwamba shughuli za uchukuzi katika barabara hiyo hazivurugiki. Malori yataruhusiwa kuendelea na safari zao kwenye barabara hiyo kuanzia saa moja jioni ya leo.

 

Baada ya zaidi ya miaka 96 duniani hatimaye safari ya hayati rais mtaafu Daniel Toroitich Arap Moi inafika tamati hivi leo.

Moi anazikwa leo nyumbani kwake Kabarak katika kaunti ya Nakuru. Maombi ya mazishi yanaandaliwa katika shule ya msingi ya Kabarak kabla ya mwili wake kusafirishwa takriban kilomita nne hadi nyumbani kwake atakapozikwa mkabala na marehemu mkewe Lena Moi aliyefariki mwaka 2004.

 

Mamia ya watu walianza kufika katika shule ya msingi ya Kabarak kuanzia mwendo saa kumi asubuhi tayari kumpa mkono wa buriani mwenda zake rais mutaafu. Kila alipowasili alipokezwa mkate na maji.

 
Toa comment