MB DOGG ATOBOA SIRI YA KUPOTEA, NCHI ALIYOKIMBILIA

Mohammed Ally ‘Mb Dogg’

KWA wale waliokuwa wakipenda kusikiliza Muziki wa Bongo Fleva miaka ya 2006 watakuwa wanaelewa mashairi ya ngoma hii ya Si Uliniambia iliyoimbwa kwa ufundi miaka hiyo na Mohammed Ally ‘Mb Dogg’ ukipenda waweza kumuita Man Dogg.

Jamaa alikuwa anaujua muziki, alikuwa anajua kucheza na sauti hasa katika nyimbo za mapenzi na ndiyo maana wengi waliobahatika kusikiliza ngoma zake kuanzia Latifa, Natamani, Inamaana na Sagaplasha walimbatiza jina la king wa makopakopa.

Mb Dogg alikuwa mmoja kati ya vichwa hatari kutoka Lebo ya Tip Top Connection iliyokuwa na vichwa vingine enzi hizo kama vile Keisha, Madee, Spack, Z Anto na wengine kibao.

Baada ya kutamba miaka hiyo, ghafla alizima kwenye muziki akiwa bado wa moto, baada ya miaka zaidi ya sita aliibuka tena na Ngoma ya Mbona Umenuna na Sio Siri ambazo nazo hazikufanya poa akatulia na kutoa Ngoma ya Uwe Wangu kisha akakaa kimya tena.

Star Showbiz limemtafuta na kufanya naye mahojiano Exclusive kuhusiana na maisha na muziki wake, ungana naye;

Star Showbiz: Kwa kipindi chote hicho ulikuwa wapi?

Mb Dogg: Nipo wakati mwingine huwa natoka nje ya nchi mishen’tauni si unajua dunia inazunguka hii huwezi kukaa sehemu moja, kwa hiyo naweza nikasema nipo kwa sababu napatikana wakati wote.

Star Showbiz: Kwa hiyo ulikuwa unajishughulisha na nini kwa ajili ya kuendesha maisha yako?

Mb Dogg: Biashara zangu tu tofauti tofauti, huwa nafanyia Kenya na Sauz (Afrika Kusini), maana huko kuna familia yangu na marafiki zangu, kwa hiyo mara nyingi huwa nakuwa huko.

Star Showbiz: Kwa nini uliacha ghafla muziki ukapotea?

Mb Dogg: Muziki sikuacha jumla ila kuna muda unaweza ukafanya halafu wewe mwenyewe ukaona kuna uzito f’lani hivi upepo ulipotea lakini pia kulikuwa na mambo nje ya ramani ambayo pia sikuwa tayari kuyazungumza yalinifanya kwanza nirudi nyuma lakini kwa sasa naamini muda sio mrefu mazoezi yatafanyika na mashabiki watanisikia nilikuwa nafanya nini.

Star Showbiz: Ulikuwa na menejimenti?

Mb Dogg: Ndio nilikuwa chini ya Kampuni ya QS Mhonda ambayo ilikuwa inasimamia katika kila kazi yangu lakini sema mkuu wa kampuni hiyo ambaye alikuwa kama mlezi wangu naye akaondoka nje ya nchi kutokana na kuwa na kampuni kubwa huko anaisimamia kwa hiyo nikawa nipo tu kishida shida ndio maana nikaamua nisimame kwanza.

Star Showbiz: Kwa hiyo unavyorudi kwenye gemu umeshapata menejimenti mpya au utakuwa unajisimamia mwenyewe?

Mb Dogg: Nimepata menejimenti mpya kuna mtu aliniomba baada ya kuona nipo kimya muda mrefu akaniambia yeye ni shabiki wangu na angependa kuniona nikiendelea na muziki. Akaomba tuonane ili tuweze kuongea na kuafikiana baadhi ya mambo bado hatujayaweka sawa na yakiwa vizuri mtanisikia rasmi.

Star Showbiz: Umejipanga vipi juu ya ujio wako wa sasa na upepo wa muziki unaofanywa sasa?

Mb Dogg: Hizi chaki unajua nilizishika mwenyewe mwanzo kwenye ubao na kufundisha watu muziki pale Tip Top na kutoa wasanii wakubwa tu labda nijipange na instrumental maana zimekuwa za kigeni na watu wamejaribu kubadilisha baadhi ya vitu ila niwaahidi bado niko vizuri.

Star Showbiz: Unautofautishaje muziki uliokuwa unaufanya na wa sasa?

Mb Dogg: Siwezi nikafanya mlinganisho kwa sababu muziki niliokuwa nafanya hakuna ambaye ameweza kuufanya hata baada ya mimi kuwa kimya kwa muda, muziki wangu ni wa kipekee na ndio maana haijawahi kusikika mtu anaimba kama Mb Dogg kwa sababu niko kitofauti sana.

Star Showbiz: Umeoa?

Mb Dogg: Ndio nimeoa na nina watoto pia japo siwezi kusema ni wangapi maana si unajua upepo wa sasa wa kutekana tekana naomba nisiwataje kwa usalama wao ila jua tu kuwa nina watoto.

Star Showbiz: Wasanii wa sasa wanafanya kiki kwa ajili ya kubusti muziki wao, vipi na wewe utakuwa unafanya hivyo?

Mb Dogg: Hapana! Muziki wangu unajibusti wenyewe na ndio maana zamani hakukuwa na mambo ya kiki lakini tulikuwa tunafanya vizuri bado kwa hiyo kiki mimi hainibariki kabisa yaani.

Star Showbiz: Kitu gani ambacho watu hawakijui kutoka kwako?

Mb Dogg: Wasichokijuwa kwangu mimi ni mchoraji mzuri sana wa ramani za majumba na ndio napiga hela huko na nimeajiriwa kwenye kampuni kabisa inayohusika na hayo mambo.

Star Showbiz: Asante kwa muda wako.

Mb Dogg: Asante na wewe pia, karibu!

 STORISHAMUMA AWADHI

Loading...

Toa comment