Mbatia: Mimi Bado ni Mwenyekiti Halali wa NCCR-Mageuzi
MWENYEKITI aliyesimamishwa wa Chama Cha NCCR- Mageuzi James Mbatia amesisitiza kuwa yeye bado ni Mwenyekiti halali wa Chama cha NCCR- Mageuzi licha ya amri iliyotolewa na Kaimu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Sisty Nyahoza
Mbatia ameyasema hao wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari akidai kwamba mfumo mzima wa uendeshaji wa masuala ya vyama vya kisiasa inaendeshwa kiumbea umbea, kimajungu majungu na fitina hali iliyomfanya aibuke na kusema ili kuokoa mtafaruku na sintofahamu inayojitokeza baina ya wanachama wa NCCR- Mageuzi.
Mbatia amethibitisha kupokea taarifa ambayo inadaiwa kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini lakini taarifa hiyo inaonekana ni ya mwaka jana mwezi wa tano hivyo ili kuthibitisha uhalali wa taarifa hiyo alimtafuta msajili msaidizi wa vyama vya siasa nchini Sisty Nyahoza ambaye hakupokea simu yake.
Mbatia aliamua kumpigia simu Msajili wa Vyama Jaji Francis Mutungi ambaye alimjibu yupo Dodoma Kikazi lakini naye pia alikiri kuwa taarifa za kuhusu NCCR-Mageuzi zinamchanganya.
“Nikaamua kumpigia Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi ambaye yeye ndiye mwenye mamlaka haya lakini akanijibu yupo Dodoma akaniambia nanukuu maneno ya Jaji Mutungi akaniambia hizi taarifa za NCCR hata mimi zinanichanganya ninakuja Dar es Salaam kesho tutawasiliana.” Alisema Mbatia.
Amebainisha kuwa hata kikao alichosikia kuwa kimekaa kurasini yeye hajui chochote nay eye ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.
Mbatia alimaliza kwa kusisitiza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mujibu wa Katiba ya NCCR- Mageuzi, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa na kanuni nyingine zote yeye ni Mwenyekiti halali wa NCCR-Mageuzi