The House of Favourite Newspapers

Mbelgiji Abadili Mfumo Simba

Mbelgiji, Patrick Aussems (kulia).

MAMBO ni moto katika kikosi cha Simba huko nchini Uturuki ambako kikosi hicho kinachoendelea kujifua kwa ajili ya msimu ujao, ambapo moja ya mabadiliko yaliyopitishwa na kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems ni katika mfumo wa mawasiliano.

 

Unaambiwa kuwa mawasiliano yoyote ya kiofisi kuhusiana na timu kutoka kwa viongozi kwenda kwake ni lazima yawe kwa maandishi na yatumwe kwake kwa njia ya barua pepe (email) lakini pia nakala zitumwe kwa viongozi wengine wa juu yake.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Ijumaa limezipata zimedai kuwa utaratibu huo wa Aussems unaonekana kuwa mpya kwa baadhi ya viongozi kutokana na kuonekana kuwatesa.

 

“Huo ndiyo utaratibu mpya wa mawasiliano ya ndani ya timu yetu ambao kocha amependekeza utumike, kwa hiyo na sisi hivi sasa tunajitahidi kuufanya, hivyo japokuwa unatusumbua kidogo kwa sababu tulikuwa hatujauzoea.

 

“Kwa mfano tunapotoka mazoezini, daktari anatakiwa kuandika ripoti yake inayoonyesha afya za wachezaji na maendeleo ya wachezaji ambao ni majeruhi kisha amtumie kwa njia ya email huku nakala akituma kwa viongozi wengine ambao wanastahili kupata ripoti hiyo.

“Kwa hiyo na viongozi wengine wote wanatakiwa kufanya hivyo kwa ajili ya kulinda maslahi ya timu na kuondoa hali ya kuingiliana katika kufanya maamuzi,” kilisema chanzo hicho cha habari na kukiri kuwa mfumo huo umekuwa ukiwapa wakati mgumu watendaji kwa kuwa hayakuwa mazoea yao.

 

Alipoulizwa kuhusiana na hilo Meneja wa Simba, Richard Robart ambaye yupo na kikosi hicho nchini Uturuki hakuwa tayari kusema chochote zaidi ya kudai kuwa hayo ni mambo ya ndani ya timu kwa hiyo hawezi kuyazungumzia.

 

KUINGIA UWANJANI LEO

Wakati huohuo, kikosi cha Simba kinatarajiwa kushuka uwanjani leo Ijumaa majira ya kumi alasiri kukipiga dhidi ya mabingwa wa sasa wa Ligi Kuu ya Morocco, Ettihad Riadi De Tanger.

Timu hizo zitacheza mchezo huo wa kirafiki nchini Uturuki ambapo zote zimeweka kambi nchini humo kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao wa 2018/19.

 

Ofisa Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara amesema kuwa mchezo huo utakuwa ni muhimu kwa timu zote kwa kuwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya na utakuwa na faida kwa pande zote mbili.

 

IR Tanger walitwaa ubingwa wa msimu uliopita wakifuatiwa na Wydad Casablanca huku Difaâ El Jadidi ambayo Mtanzania, Simon Msuva anaichezea ikimaliza ligi kwa kushika nafasi ya tano.

 

Akizungumzia michezo hiyo ya kirafiki Aussems alisema: “Kwangu mimi na benchi la ufundi ni sehemu ya mazoezi lakini wachezaji watacheza kama mechi na wanatakiwa kufurahia. Tumekuwa tukifanya mazoezi mara mbili kwa siku, hiyo itatusaidia kujua mambo kadhaa ya kimbinu.”

 

Awali, juzi Simba ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Moulodia Oudja ya Morocco uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 katika kiwanja cha Hoteli ya The Green Park kilichopo katika mji mdogo wa Kartepe, Kocael.

Bao la Oujda lilifungwa dakika ya 55, la Simba lilifungwa na Adam Salamba dakika ya 58 huku mchezo ukimalizika dakika ya 65 kutokana na mvua kubwa.

Simba pia inatarajiwa kushuka uwanjani kesho Jumamosi kucheza na moja ya timu za Uturuki kisha keshokutwa Jumapili wanatarajiwa kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya Tamasha la Simba Day ambapo watacheza na Asante Kotoko ya Ghana.

Comments are closed.