The House of Favourite Newspapers

Mbelgiji Aitisha Kikao Kizito…

0


BAADA ya sare tatu za mfululizo kwenye Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael, jana usiku ameitisha kikao cha dharura cha wachezaji wake wote kwa ajili ya mastaa hao kujitathimini ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ya ushindi katika michezo ijayo.

 

Yanga hivi karibuni ilifanikiwa kuambulia sare tatu za mfululizo katika Ligi Kuu Bara walipocheza dhidi ya Mbeya City, Tanzania Prisons na Polisi Tanzania huku ikiwaacha watani wao wa jadi, Simba wakipata ushindi katika michezo yao na kuendelea kuongoza katika msimamo.

 

Wakati kocha huyo akiitisha kikao hicho, keshokutwa Jumapili timu hiyo inatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga kuvaana na Coastal Union mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani kutokana na kila timu kuhitaji ushindi.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa kutoka kwenye kambi ya timu hiyo iliyoweka mkoani Tanga, kocha huyo jana asubuhi aliwataka wachezaji kufanya kikao cha peke yao na kikubwa kujitathimini ili kuhakikisha katika mchezo dhidi ya Coastal utakaopigwa kuanzia saa 10:00 kamili, wanaibuka na alama tatu.

 

Mtoa taarifa huyo mwenye ushawishi katika timu hiyo, alisema kuwa kocha huyo amewataka wachezaji hao kuwatathimini wadhamini wao GSM wanaotumia mamilioni kwa ajili ya kulipa posho kwa wakati.

 

Aliongeza kuwa baada ya kikao hicho ataomba mrejesho wa taarifa kutoka kwa manahodha wake, Mkongomani Papy Tshishimbi na Juma Abdul ili kujua walichokubaliana katika kikao hicho ambacho kilitarajiwa kufanyika usiku wa kuamkia leo.

 

“Kama kocha yeye ametimiza majukumu yake ya kufundisha kwa maana ya kuandaa timu, lakini tatizo lililopo ni kwa wachezaji kushindwa kutimiza majukumu yao ya uwanjani wakiwemo washambuliaji ambao wenyewe wanapata nafasi nyingi za kufunga lakini wanashindwa kuzitumia.

 

“Hivyo, kama kocha yeye amewataka wachezaji kufanya kikao mara baada ya chakula cha leo (jana) jioni wakitokea katika mazoezi ya mwisho wakijiandaa na mchezo dhidi ya Coastal.

 

“Na kikubwa kocha anataka kuona kila mmoja akitimiza majukumu yake ya uwanjani ikiwemo mabeki kuokoa hatari golini, viungo kuchezesha timu na washambuliaji kufunga mabao kwa kuanzia mchezo dhidi ya Coastal,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Abdul ambaye ni nahodha wa timu hiyo kuzungumzia hilo alisema: “Kama wachezaji tumekuwa tukiumizwa na matokeo hayo ya sare ukiangalia hivi sasa timu inalipwa mshahara na posho kwa wakati, hivyo inapotokea timu haipati matokeo mazuri tunaumia sana.

 

“Hivyo, kama wachezaji tutakutana kuzungumza na kikubwa kuwekeana makubaliano mazuri ya kupata ushindi katika michezo inayofuata ukiwemo dhidi ya Coastal.”

Leave A Reply