The House of Favourite Newspapers

Mbelgiji: Al Ahly walitumaliza dakika 45 tu

BAADA ya kupokea kichapo kikali cha mabao 5-0 wakiwa ugenini nchini Misri mbele ya Al Ahly, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amefunguka kwamba kila kitu kwenye mechi hiyo kiliishia dakika 45 za kwanza tu.

 

Simba juzi Jumamosi walikutana na kichapo hicho kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Makundi ukiwa ni mchezo wa Kundi D. Hiki ni kichapo cha pili kwa Simba wanapokea kwa kufungwa mabao 5-0 msimu huu kwenye hatua hiyo, baada ya wiki chache kufungwa na AS Vita Club ya DR Congo.

 

Kocha huyo raia wa Ubelgiji, ameliambia Championi Jumatatu, kuwa hesabu zao katika mechi hiyo zilimalizika baada ya wao kuwaruhusu Al Ahly kuwafunga mabao mengi ndani ya kipindi cha kwanza pekee.

 

“Unaporuhusu kufungwa bao la mapema mbele ya timu kama Al Ahly ni lazima iwe ngumu kwako kupata matokeo, kikosi changu kilikuwa na shida katika beki wa pembeni na viungo.

 

“Niwapongeze Al Ahly, walifanya kazi yao vizuri na ndiyo maana wakashinda, lakini pia wao ni wazuri kuliko sisi. Kwetu mechi iliisha mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza pekee ambapo tulikuwa tumesharuhusu mabao mengi.

 

“Wakati tukiwa katika vyumba vya kubadilishia nguo niliwaambia wachezaji kufungwa 5-0 ni sawa na mechi imeisha, sasa inabidi tuwaonyeshe soka kwa kuwa hatukuwa na la kupoteza kwenye kipindi cha pili ndiyo maana tukacheza vizuri kuliko hata kipindi cha kwanza,” alisema kocha huyo.

Said Ally, Dar es Salaam

Comments are closed.