The House of Favourite Newspapers

Mbelgiji Simba Aomba Siku 14 Kusuka Kikosi

KUTOKANA na Simba kutengeneza nafasi nyingi katika mechi wanazocheza ligi kuu na kushindwa kuzitumia vizuri, Kocha Mkuu wa Simba, raia wa Ubelgiji, Patrick Aussems, amesema kuwa anahitaji wiki mbili kuweza kusuka kikosi bora.

 

Simba wamecheza mechi 7 huku wakiwa na idadi ya mabao ya kufunga nane huku wakifungwa mabao matatu, licha ya kuwa na washambuliaji wengi wa kimataifa jambo ambalo kocha mkuu halimfurahishi.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Aussems alisema kuwa kikosi cha Simba ni kipana na kina wachezaji wengi wazuri ambao wanahitaji kuongezewa ujuzi zaidi na kuweza kuwafanya wacheze kwa kuelewana hasa katika safu ya ushambuliaji.

 

“Tuna wachezaji wengi wazuri ambao wanahitaji kupewa ujuzi zaidi, hasa wa kutumia nafasi ambazo wanazipata katika mashindano ambayo tunashiriki, hivyo baada ya kukaa nao kwa muda wa wiki mbili, ninaamini nitakuwa na kikosi kizuri.

 

“Kwa sasa nina wachezaji kama akina Salamba (Adam), Niyozima (Haruna) ambao wanaweza kufanya mambo makubwa kwenye timu ila ni jambo la kusubiri tu wakati ili waweze kuwa katika ubora wao, taratibu tunaanza kuondoka kwenye tatizo la kutumia nafasi, hatuwezi kutoka ghafla tu, linahitaji muda,” alisema Aussems.

Lunyamadzo Mlyuka, Dar es Salaam.

Comments are closed.