The House of Favourite Newspapers

Mbeya City yashusha majembe mapya tisa

0

mbeya city
Hans Mloli, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Mmalawi, Kinnah Phiri amedhamiria kukijenga upya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao baada ya kuhitaji saini za wachezaji wapambanaji wapya tisa kikosini hapo.
Mbeya City iliyomaliza ligi ikiwa kwenye nafasi ya nane imethibitisha kuhitaji kurejea kwenye kiwango chake katika msimu ujao hivyo sasa inapambana kupata wachezaji hao wanaoaminika kurejesha makali ya timu hiyo kwa msimu ujao.
Akizungumza na Championi Jumatano, Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe amefafanua kuwa, wamepanga kufanikisha usajili huo kwa ajili ya kutekeleza maagizo ya ripoti ya Phiri kwa ajili ya kusuka timu hiyo iliyoanza kupoteza makali yake kwa sasa.
Aidha, katika wachezaji hao tisa, Kimbe ametaja kuwa wanahitajika mastraika watatu, viungo wawili, mabeki wa kati wawili na mabeki wa pembeni pia wawili.
“Kocha anahitaji kusuka kikosi kizuri zaidi msimu ujao, kwa hiyo sasa tupo kwenye mchakato wa kuangalia hizo nafasi tisa alizoziorodhesha, usajili utakuwa na kipindi kirefu kwa hiyo tuna wakati mzuri wa kuchagua watu sahihi zaidi kwa ajili ya mafanikio ya msimu ujao,” alisema Kimbe.
Tayari Mbeya City imeshaonyesha nia ya kumnyakua mshambuliaji wa Azam FC, Mrundi, Didier Kavumbagu ili kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji huku taarifa nyingine zikieleza mahesabu yao pia ni  kumsajili straika wa Ndanda FC, Atupelle Green.
Katika eneo la kiungo, mpaka sasa anayetajwa kuwa kwenye rada za timu hiyo iliyoshiriki misimu mitatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara ni kiungo wa Toto Africans, Abdallah Seseme.

Leave A Reply