MBINU ZA KUKABILIANA NA TATIZO LA UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME

ZAMANI matatizo ya unyumba hayakuwa hadharani, yalikuwa ni siri ya mke na mume. Matatizo ya unyumba ni mambo ya chumbani, kutokana na utandawazi matatizo haya sasa yapo hadharani, hii ni kutokana na matatizo ya ndoa kuwa makubwa na kuwaathiri wote, mwanamke na mwanaume.  Katika kukabiliana na changamoto hizi au matatizo haya ya upungufu wa nguvu za kiume, wataalam wa afya wameweza kuchunguza vyanzo na kujua suluhisho la tiba za tatizo hili ambalo hutibika mahospitalini tu siyo sehemu nyingine. Zipo njia mbalimbali ambazo kwa mtu yeyote mwenye tatizo hili anaweza kuzifuatilia na kupata ufumbuzi.

Madaktari wanafafanua kuhusu upungufu wa nguvu za kiume ni kwamba, mwanaume anashindwa kusimamisha uume wake kwa muda wote wa tendo la kujamiiana au uume kushindwa kusimama anapohitaji kushiriki tendo hilo. Kutokana na tafiti mbalimbali inaonesha kwamba tatizo la upungufu wa nguvu za kiume linaathiri takriban wanaume wengi kati ya milioni 15 hadi milioni 30 duniani kote.

Tatizo hili hutokea kufuatana na umri na zaidi huanza umri wa miaka 40 na katika umri huu asilimia tano ya wanaume huathirika. Tatizo huongezeka zaidi hasa pale umri unapoanzia miaka 65 ambapo tatizo huongezeka kwa asilimia 15 hadi 25.

Tatizo linapotokea katika umri wa chini ya miaka 40, basi inaweza kuwa ni tatizo kubwa linalohitaji uchunguzi wa kina. Vipo vipindi tofauti ambavyo kila mwanaume anapitia kwa muda mfupi kuhisi upungufu wa nguvu za kiume ambapo baada ya muda hukaa sawa hata bila kutumia dawa.

NJIA ZA KUKABILIANA NA TATIZO

Kwanza, pata muda wa kujiandaa kabla ya tendo, kadiri mwanaume umri unapoongezeka au unapozidi kuwa mzee msisimko wa mapenzi unapungua, hivyo utahitaji muda mrefu wa kujiandaa au kuandaliwa ili msisimko usogee. Jambo la msingi ni wewe mwenyewe kuwa na subira na kuvuta hisia taratibu hadi unakaa sawa.

Katika umri wa miaka 18 hadi 20 kwa mwanaume, msisimko huwa mkubwa sana, katika umri wa miaka kati ya 30 na 40 hapa msisimko huanza kupungua taratibu labda kutokana na majukumu kuanza kuongezeka. Kadiri umri unavyoongezeka nguvu huanza kupungua, haina maana ni tatizo au ugonjwa kama una afya nzuri. Muda tangu tendo la kwanza hadi la pili huongezeka kadiri umri unavyoongezeka.

Kwa kawaida kutoka tendo moja hadi lingine huchukua saa sita hadi nane ukiwa na umri wa chini ya miaka 40, lakini kadiri umri unavyoongezeka, muda huo huongezeka hadi kufikia saa kumi na mbili. Mwanaume kuanzia miaka sitini muda unaweza kuwa mrefu zaidi kutoka saa kumi na mbili hadi 72 hivyo inatakiwa ujue muda zaidi wa kuvuta hisia taratibu na muda mwingi uwe na mwenzio akikuandaa hadi uwe tayari. Hapa inamaanisha kwamba mwanaume pia inatakiwa aandaliwe vizuri ‘romance’ kabla ya tendo na siyo mwanamke pekee ndiye anayeandaliwa. Wanaume baadhi hupungukiwa uwezo wa kufanya tendo hili kwa kutopata ushirikiano mzuri kutoka kwa wake zao. Hivyo basi hili siyo tatizo bali ni hali ya kimaumbile ambayo inaweza kurekebishwa.

Jambo jingine ni kuangalia dawa unazotumia. Baadhi ya madawa huchangia kupunguza nguvu za kiume, mfano; dawa za presha na baadhi ya madawa ya magonjwa sugu. Nakushauri umwone daktari wako akushauri kuhusu hizo dawa unazotumia. Magonjwa sugu kama magonjwa ya moyo, kisukari, kifua kikuu, kansa na mengine mengi yanaweza kusababisha tatizo hili.

Achana na matumizi ya kilevi, unywaji wa pombe ni hatari kiafya kwa hiyo angalia unywaji wako wa pombe, hakuna kiwango kizuri cha pombe kiafya, pombe ina madhara hata kwa kiwango kidogo, pombe inapunguza uwezo wa mwili na akili, mtu anakuwa mzito kutenda au kufikiri. Kwa mujibu wa mwanafalsafa maarufu wa karne zilizopita, Shake Spear, katika suala la mapenzi, pombe huamsha hisia na hamasa za kushiriki tendo, lakini huondoa uwezo wa kulitenda tendo hilo (alcohol provokes desire but takes away the performance).

Kwa kawaida pombe husababisha kusinyaa kwa mfumo wa mishipa ya fahamu (alcohol is a nervous system depressant) na kusababisha kuondoa msisimko wa kimapenzi hata kama una hamu ya kutosha. Pombe, ili kuleta athari mwilini haihitaji unywe kiwango kikubwa, hata glasi mbili tu, zinaweza kuharibu mfumo wa fahamu na ini.

Itaendelea wiki ijayo.

Loading...

Toa comment