The House of Favourite Newspapers

MBINU ZA KUMFANYA AAMINI KAMA KWELI UNAMPENDA KWA VITENDO-2

WIKI iliyopita nilianza kuichambua mada hii kama inavyosomeka hapo juu. Narudia tena kusisitiza, kumwambia I Love You nyingi mpenzi wako wala siyo kigezo cha kumfanya aamini kwamba unampenda kwa sababu wahenga walisema maneno matupu hayavunji mfupa.

Hii pia inakuhusu wewe ambaye unahangaika kutaka kujua kama uliye naye anakupenda kweli au anakutamani? Maneno pekee hayatoshi kukufanya umuamini, bali vitendo ndivyo huzungumza zaidi.

Wiki iliyopita tuliangalia mbinu tatu za awali za kumfanya aamini kwamba unampenda, ambazo ni kumsaidia pale anapokuwa na uhitaji bila masharti yoyote, kumpa kipaumbele na kuwaonesha watu wengine kwamba unampenda na unajivunia kuwa naye.

Leo tunaendelea na mbinu zilizosalia:

  1. WAPENDE NDUGU ZAKE

Watu wengi huwa wanajidanganya kwamba ndugu hawawezi kuingilia mapenzi. Ukweli ambao wengi hawaujui, ni kwamba hata kama ndugu kweli hawawezi kuingilia au kuharibu uhusiano wa kimapenzi uliomo ndani yake, lakini ukiwachukia ndugu wa umpendaye, tafsiri ni kwamba hata mapenzi yako kwake yana walakini.

Unawezaje kumpenda mtu halafu ukamchukia mama yake aliyemlea mpaka akawa mkubwa na kukutanana wewe? Ninachotaka kukwambia hapa, migongano kati yako na ndugu wa umpendaye haikwepeki lakini unachotakiwa kukifanya, ni kujua namna ya kuishughulikia. Waoneshe upendo, wajali, wasaidie kama unao uwezo huo, utaona jinsi mwenzi wako atakavyozidisha mapenzi kwako.

  1. MUUNGE MKONO KWENYE SHUGHULI ANAYOIFANYA

Hii inawahusu wote, wanawake na wanaume, unakuta mtu anampenda mtu fulani lakini havutiwi na aina ya shughuli anayoifanya ili kujiingizia kipato. Unaamini kwamba kazi anayoifanya ni ya kichovu na pengine ungependa awe bosi kwenye kampuni fulani kubwa au afanye kazi benki ndiyo umuone kuwa na maana.

Hata kama anauza mkaa au anashona viatu, anauza genge au anafanya biashara ndogondogo, muunge mkono kwenye kile anachokifanya badala ya kumdharau au kumkatisha tamaa.

Wapo pia wanaume ambao anakwambia wazi kabisa hawezi kumpenda mwanamke asiye na kazi inayoeleweka! Hata kama anauza maandazi au vitumbua, muunge mkono na kama kazi anayoifanya huifurahii, wewe ndiye mwenye jukumu la kumbadilisha na hii inawahusu wote wawili.

Jivunie kuwa naye kwa sababu sifa za nje huweza kubadilika wakati wowote, bosi anaweza kufilisika na kurudi kuwa mbangaizaji mitaani na muuza mkaa anaweza kutoboa na kufungua kampuni yake, ni suala la nafasi tu.

  1. MUONESHE UAMINIFU KWA ASILIMIA 100

Tatizo kubwa la wanandoa au wapenzi mpaka wanafikia hatua ya kuachana, huwa ni usaliti. Nimeshawahi kuzungumza huko nyuma kuhusu athari za usaliti lakini ninachotaka kukwambia leo, hata kama utamfanyia kila kitu umpendaye, aiku atakapogundua kwamba unamsaliti, yote uliyoyafanya yatakuwa sawa na kazi bure.

Hata kama ataendelea kuwa na wewe, hawezi kukupenda tena wala hawezi kuamini kama unampenda, hata utamke neno I Love You mara milioni mia moja. Hii ni kwa sababu dhambi ya usaliti huwa na maumivu makali sana kwenye mapenzi, ndiyo maana hata baadhi ya vitabu vya dini vinaeleza kwamba usaliti ni kosa ambalo likitokea na mkashindwa kuelewana, mnaruhusiwa kupeana talaka.

  1. PATA MUDA WA KUTOSHA WA KUWA NAYE

Pilikapilika za maisha zinafanya watu wakose hata muda wa kukaa karibu na wapenzi wao, ukiamka asubuhi unawahi kwenye majukumu ya kila siku, ukirudi tayari ni usiku sana, umechoka, mwenzi wako naye amechoka! Mkiendelea kwa ratiba hii, hata ushiriki wenu kwenye tendo la ndoa ambalo kimsingi ndiyo linalowaunganisha, utakuwa mdogo na hata hisia za mapenzi kati yenu zitakufa.

Kwa hiyo jambo la msingi la kufanya, hata kama una ratiba ngumu kiasi gani, lazima utenge muda wa kutosha wa kukaa na mwenzi wako, mzungumze kuhusu mustakabali wa maisha yenu lakini pia mpate muda wa kutosha wa kupeana haki ya msingi ya ndoa inayowaunganisha.

Ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.

Comments are closed.