The House of Favourite Newspapers

Mbinu za kumfunga breki mwanaume anayechepuka-2

NI siku nyingine ninapo-kukaribisha msomaji wangu kwenye ukurasa huu murua, mada tunayoijadili ni ile tuliyoanza nayo wiki iliyopita, ni juu ya mbinu za kumfunga breki mume au mpenzi anayechepuka hovyo.  Tuliona kwamba ili mwanaume akupende zaidi, ni vizuri sana kuchunga kauli zako unapokuwa naye. Epukana na kauli za kisharishari muda wote, epuka kejeli, kashfa na matusi unapokuwa naye. Mfanye awe rafiki yako, piga naye stori, muulize kuhusu malengo yake katika maisha yenu na hakika, mawazo ya kukusaliti hayatakuwa na nafasi kwenye moyo wake.

Nilikwambia pia kwamba suala jingine ni uaminifu, jitahidi kuwa muaminifu na mkweli kwake kadiri unavyoweza. Maisha ya siku hizi ni magumu sana, sasa ukiwa na chembechembe za usaliti ndani yako, maana yake unamfanya kila anapokuwa mbali na wewe, badala ya kufikiria kutafuta fedha, awe anawaza kwamba sijui sasa hivi anazungumza na nani au anawaza kunisaliti kwa nani.

Matokeo yake, hawezi kukupenda, atajiona ni kama amebeba mzigo wa misumari kwenye kichwa chake na endapo atapata mtu ambaye anamuonesha tabia za tofauti na wewe, hesabu maumivu.

Tuendelee na mbinu nyingine ambazo ukizifuatilia kwa makini, hakika suala la usaliti utabaki kulisikia kwa wenzako tu.

WAHESHIMU WAZAZI WAKE

Hii inawahusu wale ambao bado wazazi wao wapo hai, kama wameshatangulia mbele za haki, basi lazima wapo watu ambao anawaheshimu na anawaona kuwa kila kitu kwake. Makosa wanayoyafanya wanawake wengi, wanaamini kwamba mwanaume akishakupenda basi inatosha, hata kama wazazi wake hawakukubali haiwezi kuathiri chochote kwenye uhusiano wenu.

Yawezekana ukawa na tofauti na wazazi wake, malalamiko mengi ya wanandoa siku hizi utasikia ‘wakwe zangu hawanipendi!’ Nasisitiza, hata kama hawakupendi, bado ni jukumu lako kuwaheshimu, kuwaonesha ukaribu na kuwapa misaada midogomidogo pale inapobidi.

Hakuna jambo linalomfanya mwanaume ajisikie vizuri, kama kuwaheshimu na kuwajali wazazi wake na ndugu zake, jifanye mjinga ili ndoa yako iendelee kuwa na amani, ukifanya hivyo hakika mumeo atakupenda na hataona sababu ya kutoka nje.

EPUKA VISINGIZIO

Hili linaweza kuwa tatizo linalosababisha usaliti uzidi kuwa janga katika maisha ya wanandoa wengi. Hapa nazungumzia visingizio mwenzako anapokuhitaji faragha. Yawezekana kwamba unachoka sana kwa kazi za kutwa nzima, lakini amini nakwambia, tabia ya kila siku kusingizia ‘nimechoka’, ‘sijisikii vizuri’, ‘kichwa kinauma’ au ‘tumbo linauma’ mwenzako anapokuhitaji faragha, ni sumu mbaya sana katika uhusiano.

Usipomtimizia wewe mahitaji yake, unataka nani afanye kazi hiyo? Hata kama umechoka namna gani au kweli unajisikia vibaya, mpe haki yake na kama ukishindwa kabisa, jenga mazingira ambayo yatamfanya hata yeye mwenyewe ajue kweli leo mke wangu ametingwa. Achana na visingizio kwani unamkaribisha shetani wa usaliti ndani ya nyumba yako.

Ukiwauliza wanaume wengi waliofikia hatua ya kutoka na mahausigeli wao au waliolowea kwa michepuko, watakueleza kwamba sababu kubwa ni kwamba walikuwa wakitafuta kile walichokikosa kwa wake zao.

Nasisitiza tena, mtimizie mahitaji yake kila inapobidi, tena wakati mwingine siyo lazima yeye ndiyo akuanze, unaweza kuwa unamfanyia ‘sapraizi’ wakati ambao pengine hakutegemea. Hakuna mwanaume anayeweza kutamani kwenda nje wakati asubuhi amepewa haki yake ndani au wakati jana alipewa haki yake mpaka akachoka mwenyewe.

Ni hayo tu, ukizingatia kwa makini hakika shetani wa usaliti utamsikia kwa wenzako tu. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Comments are closed.