TUPO kwenye sehemu ya mwisho ya mada yetu, tukiangalia vitu ambavyo huwavutia zaidi wasichana. Lengo la mada hii ni kuwasaidia wavulana kuelewa hisia za wasichana na kuzishika. Ukweli ni kwamba ukikijua kitu, hakikupi shida tena. Ndivyo ilivyo hata kwenye mapenzi na uhusiano. Ni muhimu kuelewa mwenzako anapenda kitu gani na huchukizwa na nini ili uwe smati kwenye penzi lenu. Sasa tuendelee na vipengele vilivyosalia…
WANAPENDA KUSIFIWA
Wanaume wengi hupuuzia hili, huona kama ni jambo lisilo na maana sana kwao na wenzi wao. Hali ni tofauti sana kwa wanawake ambao hupenda kuwasifia wapenzi wao. Nitakupa mifano miwili ya namna wapenzi wanavyochukulia suala la kusifia.
MVULANA: “Ben kutana na mtu wangu wa nguvu, anaitwa Queen. Tupo tunalisongesha mdogomdogo, mengine tutayajua baadaye.
MSICHANA: “Caroline, huyu ndiye baby wangu, mwanaume ninayempenda kuliko chochote duniani. Anaitwa Lucas. Ndiye ambaye nilikupa stori yake. Hapo ni mvulana na msichana, kwa nyakati tofauti wakitambulisha wenzi kwao kwa marafiki zao. Je, umeona tofauti kati ya mwanamke na mwanaume?
Unaweza kuona hapo, mwanaume anaonekana hajali sana, hana uhakika na penzi lao wala haelewi mwelekeo wa uhusiano wake.. lakini mwanamke ni tofauti, kwani ameonyesha kujali, kupenda, kuthamini na kujivunia penzi lake. Wanaume waelewe siri hii, kwamba wanawake wanatamani kuwa na wanaume ambao wanawapa sifa zote wanazostahili wakiwa nao, lakini pia mbele za watu wengine. Unaweza kuona ni jambo dogo,kubwa kwa mwanamke.
ONYESHA MALENGO
Wanaume wengi hawapendi kuwashirikisha wanawake katika mambo yao. Wanapenda kufanya mambo yao kwa siri. Hii si sahihi. Ukitaka kumkamata mwanamke kihisia, mshirikishe kwenye malengo yako.
Hata kama hutamwambia kila kitu kwa sababu bado ni wapenzi tu, lakini kumuomba ushauri juu ya mipango yako kutaongeza hamasa ya mapenzi, atajiona mwenye nafasi kwenye mambo yako, hapo utakuwa unazidi kuongeza kete ya uhai wa penzi lenu.
KIPAUMBELE
Kuna wakati wanawake huwa na mambo yao binafsi. Kazini au kifamilia. Inawezekana akatatizika katika eneo fulani ambalo kwa namna moja ama nyingine atahitaji usaidizi wako. Ikitokea mpenzi wako akawa katika hali hiyo, msikilize.
Mathalani ana tatizo la kifamilia, amekuambia mmoja wa wazazi wake anaumwa, msaidie. Si lazima kifedha, lakini kuonesha kujali kwako tu, kutampa matumani kwamba yupo na mtu sahihi. Msikilize, mshauri panapofaa kufanya hivyo na ukiweza msaidie hata kifedha. Hiyo itazidisha upendo na uaminifu kwako.
Lakini pia hata wewe unapokuwa na jambo mshirikishe. Unaweza kushangaa jambo ambalo uliamini unaweza kulimaliza peke yako, kwa kumshirikisha likawa jepesi zaidi na mambo yakaendelea vyema. Somo kubwa hapo ni kumpa kipaumbele kwenye mambo yake na yako. Kufanya hivyo kutazidisha upendo kwenye penzi lenu.
KUTUNZA SIRI
Unapokuwa kwenye uhusiano na mwanamke, mtashirikiana kwenye mambo mengi. Siyo ajabu kuwa unajua siri zake nyingi, nawe atazijua zako.
Katika mazungumzo yenu, kuna wakati atakueleza siri zake binafsi, siri za familia yao nk. Ni jukumu lako kulinda na kutunza siri hizo. Kitendo cha kuelezwa jambo fulani, halafu anakwenda kulisikia mitaani, kinakupunguzia sifa za kuwa mume wake hapo baadaye. Kuwa na kifua kama mtoto wa kiume, tunza siri.
Wiki ijayo nitakuja na mada nyingine, USIKOSE! Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.
Comments are closed.