Mbio za Kilomita 5 Kili Marathon Zapata Mdhamini Mpya

Waandaji wa Toleo la 23 la Mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2025 leo wametangaza Benki ya CRDB kuwa mdhamini mpya wa mbio za kujifurahisha za masafa mafupi ya kilomita 5 kuelekea mashindano yenyewe yatakayofanyika Februari 23, 2025.
Taarifa iliyotolewa na waandaaji mbio hizi jijini Dar es Salaam leo, inasema wamefurahishwa na wameikaribisha Benki ya CRDB na kuongeza kwamba mbio hizi sasa zitajulikana kwa jina la CRDB 5Km. Fun Run.
Huu ni mwaka wa pili kwa Benki ya CRDB kudhamini mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Larger. Mwaka jana Benki ya CRDB ilikuwa sehemu ya wadhamini waliounga mkono mashindano hayo.
“Mbio za kilomita 5 ni mbio kubwa zinazovutia takribani wakimbiaji 5,000.

Hivyo, Benki ya CRDB, taasisi kubwa ya kifedha nchini Tanzania, imejipanga vizuri kuwa mdhamini wa mbio hizi na tunatazamia uhusiano huu utakuwa wa muda mrefu na utachukua shindano hili la mbio hadi ngazi nyingine,” anasema John Addison, Mkurugenzi wa Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Larger.
Waandaaji pia walitoa wito kwa wadhamini wengine kujitokeza kwa kutumia vizuri fursa hii.
Akizungumzia ushiriki wao, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela anasema wanajivunia kuhusishwa na mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Larger, moja ya matukio makubwa ya kimichezo nchini, ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kukuza mitindo ya maisha afya, utalii na biashara kwa jumla, hasa mkoani Kilimanjaro na kwa wakazi wa Moshi, ambako mbio hizi hufanyika kila mwaka.
“Kwetu sisi, hili ni jukwaa sahihi la kuitangaza benki yetu kwani tunatarajia kuwafikia wakazi wengi wa Moshi na maeneo ya jirani na kuwashirikisha kupitia Mbio za CRDB 5Km Fun,” anasema.

Aidha, anabainisha kwamba wanatarajia kuutalii Mji wa Moshi na kuwashirikisha wateja juu ya manufaa ya bidhaa na huduma zao kwa manufaa yao binafsi ya kiuchumi na maendeleo ya taifa.
Nsekela amewataka washiriki wa mbio za za kilomita 5 kujiandikisha kwa wingi kwani sasa wana kitu cha kutarajia kabla, wakati na baada ya mbio hizi.
“Tutatuma mabasi mengi ya wafanyakazi, wateja na waandaaji wa mbio hizi ili kushiriki na kufurahia kwa wakati mmoja,” anaongeza.
Kilimanjaro Premium Lager ndio mdhamini mkuu wa mbio za masafa marefu (mbio za kilomita 42), Yas (mbio za kilomita 21), na wadhamini wengine ni pamoja na Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies na TPC Sugar Ltd na wasambazaji rasmi ni GardaWorld Security, CMC Automobiles, Sal. Salinero Hoteli. Wengine ni Kibo Palace Hotel na Keys Hotel.
Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager zitakazofanyika Jumapili ya Februari 23, 2025 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa ndani ya nchi na Executive Solutions Limited, huku Wild Frontiers Events wakiwajibika kwa usafiri wote wa ndani na kulitangaza tukio hili kimataifa.