Mbio Za Urafiki Tanzania Na India Kurindima Dar Mpaka Bagamoyo Keshokutwa




Dar es Salaam 28 Desemba 2023: Mbio za urafiki zitakazoshirikisha wakimbiaji wa hapa nchini na India zinatarajiwa kutimua vumbi kesho Desemba 30 mpaka 31 kuanzia jijini Dar es Salaam mpaka Bagamoyo kwenda na kurudi kesho yake.
Mbio hizo zitahusisha kilometa 5 na 10 na kufuatiwa na mbio ndefu za kilometa 120 kwenda Bagamoyo mkoani Pwani na kurudi Dar es Salaam huku zikiongozwa na mwanariadha mashuhuri wa nchini India, Milind Soman.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mbio hizo, Balozi wa India hapa nchini, Binaya Srikanta Pradhan, amesema maandalizi yote ya mbio hizo tayari yameshakamilika na wanatarajia ziwe mbio za aina yake. Balozi Binaya amesema anaishukuru serikali na Watanzania waliojiandikisha kushiriki katika mbio hizo ambazo lengo lake ni kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India.
Alisema mbio hizo zitahusisha wakimbia ambao ni raia wa Tanzania na India na usaili umelishafunguliwa huku kukiwa hakuna gharama za kujiunga. Aliendelea kusema wameandaa mbio hizo kuhakikisha wanadumisha umoja uliopo kati ya nchi hizo mbili ikiwemo wanariadha mbalimbali kubadilishana mawazo.
Aliongeza Soman ambaye kwa sasa ni mkufunzi wa mbio za riadha nchini India, atapata fursa ya kuzungumza na wanariadha mbalimbali kuhakikisha wanabadilishana uzoefu.
“Umoja wa India na Tanzania tumeandaa mbio za riadha ambazo zitafanyika kuanzia Dar es Salaam hadi Bagamoyo mkoani Pwani na baadaye zitatoka Bagamoyo kurudi Dar es Salaam ambapo tutakimbia kilometa 120, pia tutakuwa na mkongwe Soman ambaye hivi sasa ni mkufunzi wa mchezo na msanii wa filamu nchini India,” alimaliza kusema Balozi Pradhan.
Naye Soman alisisitiza kwamba ameshafanya mbio kama hizo katika nchi mbalimbali na sasa ni zamu ya Tanzania na yupo tayari kukimbia. “Ni fursa nzuri kwangu kutembelea Tanzania kuja kuiongoza timu itakayoshiriki mbio za riadha kwa pamoja, ambapo tutaungana na Watanzania mbalimbali lengo ikiwa ni kubadilishana uzoefu na kudumisha utamaduni uliopo kati ya nchi hizi mbili.
“Nimeshafanya safari kama hizi katika nchi mbalimbali Ulimwenguni, sasa ni zamu ya Tanzania, kuhakikisha tunafikia malengo. “Tunafurahi na tunajivunia kuwakilisha Ubalozi wa India nchini Tanzania kupitia mbio za riadha ninafikiri tutaacha alama kwa wenyeji,” alisema Soman.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), William Kalaghe, alisema wamefarijika kuwa sehemu mbio hizo na waliunda kamati maalumu kuhakikisha wanafikia malengo. Alisema mbio hizo ni fursa ya kuutangaza mchezo wa riadha zaidi na zinatarajiwa kuwa endelevu kwani zitafungua milango kwa wadau wengi wa mchezo huo.
“Tunashukuru kwa kujumuishwa katika sehemu ya maandalizi ya mbio hizi ambazo zinafanyika hapa nchini kwa mara ya kwanza, hivyo tunatarajia zitakuwa endelevu na wanariadha mbalimbali watanufaika kupitia mbio hizi,” alimaliza kusema Kallaghe.