The House of Favourite Newspapers

Mbongo Uingereza Asimulia Alivyopona Corona

0


WAKATI maambukizi ya Virusi vya Corona yakizidi kushika kasi nchini, Mtanzania anayeishi katika mji wa Crawley nchini Uingereza, Happy Oshea ameeleza jinsi alivyopambana na maambukizi ya virusi hivyo ndani ya familia yake bila kukata tamaa.

 

Mtanzania huyo ambaye familia yake ni ya watu wanne, wote walipata maambukizi ya ugonjwa huo (COVID – 19), ambao hadi Aprili 13 watu 84,279 nchini Uingereza walikuwa wameambukizwa huku 10,612 wakifariki.

 

Akizungumza na RISASI MCHANGANYIKO kwa njia ya simu, Happy alisema ulikuwa ni muujiza wa Mwenyezi Mungu baada ya yeye kupona licha ya kwamba familia yake wanaendelea kutumia dawa za kutuliza maumivu pamoja na tiba asili nyumbani.

 

“Kwa kweli watu wanaweza kuzungumza na kuchukulia Corona kama ni jambo la kawaida, lakini napenda kuwaambia ni ugonjwa hatari sana.

“Kwa sababu kwenye familia yangu, mimi ndio nilianza kuumwa baada ya kupata dalili kama vile kuwashwa koo, kujisikia vichomi na kupata homa kali,” alisema.

 

Alisema alianza kujisikia vibaya na kupata dalili hizo kuanzia Machi 22, ndipo alipoamua kwenda hospitali na alipopima aligundulika kuwa na virusi vya Corona.

“Baada ya kugundulika nina Corona, ilibidi sasa kwenda kupima familia yangu nzima, yaani mume na watoto wawili ambao wote walibainika kuwa na maambukizi hayo.

 

“Tulipojaribu kufanya tafiti chanzo ni nini, ndipo tukagundua kuwa mume wangu ndiye aliyeanza kuambukizwa kutoka kwa mteja wake alipokuwa akisikiliza kesi yake.

 

“Yaani ni kwamba, kama yule mgonjwa angemwambia mume wangu kama ana tatizo hilo, basi wangejikinga lakini hakumwambia na mume wangu akaleta nyumbani na kuambukiza mpaka watoto, sijui niseme nini maana nilimuomba Mungu, asinipitishe kwenye mauti, bado watoto wadogo,” alisema Happy.

 

Happy alisema baada ya kugundulika nyumba nzima wameambukizwa Corona, walianza kuumwa wote na matokeo yake hata walipoenda hospitali, walipewa huduma ya dawa kama panadol na drip kisha kurudi nyumbani maana hakuna sehemu hata ya kulala.

 

“Jamani mtu unaumwa lakini inabidi urudi nyumbani kujiuguza, kitu nilichokuwa nafanya ni kunywa supu ya mbogamboga na kuwatengenezea watoto wangu chai ya kila aina ya viungo kisha naweka ndimu wanakunywa. Hiyo ndio ilikuwa kama tiba asili,” alisema Happy.

 

Alisema kuna kipindi aliumwa, mpaka akaamua kutuma picha yake nyumbani kwa wazazi wake na kuwaonyesha kuwa amekata tamaa kwa sababu aliwaficha kwa muda mrefu, ndipo ikamlazimu kuwaeleza ukweli kuwa anaumwa.

 

“Ni kweli niliumwa sana, sikuelewa na nilijua ni mwisho wa maisha yangu kabisa, ikabidi niwatumie picha kama ya kuwaaga, kwa sababu hata watoto wangu nilikuwa nashindwa kuwahudumia, nikipata nguvu ndio naamka kuwapikia uji, lakini huwezi amini, nilijitahidi na sikukata tamaa, chai na vitu vya kujenga mwili vikanisimamisha tena. Nikacheki mara ya kwanza, nikaambiwa sina, nasubiri kucheki tena. Baba na wanaye nao wanaendelea vizuri licha ya kuwa wao bado wanaumwa,” alisema Happy.

 

Mtanzania huyo alisisitiza kuwa anaumia sana kusikia Tanzania, ugonjwa unazidi kushika kasi. Hivyo, anawasihi Watanzania kuzidi kujikinga.

 

“Huu ugonjwa ni mbaya sana, umenitesa na familia yangu bado nasubiri kipimo kingine ili tujue kama umeisha, maana hata kupima tu ilihitaji ujasiri sana,” alisema Happy.

 

Hadi Aprili 13, mwaka huu, jumla ya watu 49 nchini Tanzania walikuwa wamebainika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Corona huku kati yao, watatu wakipoteza maisha.

STORI | Imelda Mtema, Risasi

Leave A Reply