The House of Favourite Newspapers

Mbowe Ajitetea, Aieleza Mahakama Hakuwepo Kwenye Maandamano

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe  ameieleza Mahakama ya Halimu Mkazi Kisutu kuwa hakuwepo kwenye maandamano ya wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakielekea kwenye ofisi za msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni.

 

Mbowe amedai hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba wakati akitoa utetezi wake dhidi ya mashitaka yanayomkabili.

Akingozwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai kuwa kama alitajwa katika mashtaka hayo ya kukataa kutawanyika basi ilikuwa ni kwa hisia kwa sababu hakuwepo eneo la tukio.

 

Amedai kuwa baada ya kumaliza mkutano wa kufunga kampeni katika uwanja wa Buibui Mwanyamala aliindoka uwanjani hapo akiongozwa na askari polisi kuelekea Makao Makuu ya Chadema Kinondoni.

Amedai siku hiyo wahudhuriaji wa Chadema wakiwa njiani walikutana na wahudhuriaji wa CCM katika makutano ya barabara ya Morocco na Mwananyamala wakiwa na mgombea wao wakisindikizwa na ngoma aina ya mdundiko.

 

Mbowe alidai kuwa wanachama hao wa Chadema walikuwa wakiongozwa na Polisi kuelekea barabara ya Morocco ambapo yeye hakujua kilichoendelea nyuma kwani aliendelea na safari yake ya kuelekea Makao Makuu ya Chadema.

 

Akizungumzia kufikishwa kwake Mahakamani Mbowe amedai kuwa kwa mara ya kwanza alipokea wito wa kuitwa Polisi kupitia mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda maalumu Dar es Salaam.

Amedai kuwa Kamanda wa Polisi alitoa wito kwa viongozi wa Chadema kuripoti polisi kuhusiana tukio hilo la maandamano.

 

Pia amedai kuwa alipata taarifa kuhusu kifo cha Akwilina Akwiline aliyepigwa risasi katika maandamano hayo kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari na kwamba Polisi inawashilikia askari kuhusu tukio hilo.

Mbowe alidai kuwa hajawahi kula njama na washtakiwa wenzake bali waliitwa kwa nyakati tofauti kwenda Polisi.

 

Mbali na Mbowe washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

 

Pia Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018, Dar.

HABARI NA DENIS MTIMA

Comments are closed.