Mbowe, Wenzake Washindwa Kujitetea Mahakamani

VIONGOZI tisa wa Chama chas Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, wameshindwa kuanza kujitetea katika kesi ya uchochezi inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa sababu mawakili wanaowatetea wanasimamia kesi Mahakama Kuu ya Tanzania.

 

Leo viongozi hao walitarajiwa kuanza kujitetea baada ya mahakama hiyo kuwakuta na kesi ya kujibu kutokana na ushahidi wa watu wanane uliofungwa na upande wa mashitaka.

 

Wakili Gaston Garubindi amedai hayo leo Jumanne Septemba 17, 2019, kuwa  kwa maelekezo aliyopewa na wakili Peter Kibatala anaomba shauri hilo liahirishwe.

 

“Wakili Profesa Safari (Abdallah) yuko Mahakama Kuu Shinyanga mbele ya Jaji Mkeha na Kibatala yuko Mahakama Kuu mbele ya Jaji Tiganga baada ya kupata wito wa dharura jana kutakiwa afike mahakamani hapo leo,” amedai wakili Garubindi.

 

Pias  amedai kwamba wakili mwingine katika kesi hiyo, Hekima Mwasipu, yuko Mahakama Kuu Tanga kwenye kesi ya madai namba 7/2019 mbele ya Jaji Mruma.

 

Sababu nyingine iliyoelezwa na Garubindi ni mshtakiwa wa pili, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na mshtakiwa wa nane, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche,  wamefiwa na ndugu zao, hivyo wanafanya taratibu za kwenda kwenye mazishi.

 

Wakili Mkuu wa Serikali, Faraji Nchimbi, alipinga sababu hizo kutokana na kutoelezwa Profesa Safari yupo katika kesi gani, sambamba na barua ya wito.

 

Kuhusu Mchungaji Msigwa na Heche kusafiri, amesema kuna haja ya kusikia kutoka kwa washtakiwa wenyewe pamoja na kupata uthibitisho ikiwemo cheti kwa ajili ya kumbukumbu ya mahakama.

 

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alieleza kutoridhishwa kuahirisha kesi hiyo kwa siku 20 na kuipanga kuendelea Septemba 24 hadi 27 na Oktoba 1 hadi 3, 2019.


Loading...

Toa comment