Mbrazil Atua na Mikwara Mizito Simba Awapa Makavu Wachezaji Wake
KOCHA Mkuu wa Simba, Mbrazil, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amefunguka kuwa anataka kuona wachezaji wa timu hiyo wanacheza kwa kujituma na soka la kasi ili kuweza kufanya vizuri zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na wapinzani waliopangwa nao.
Robertinho ambaye alitarajia kutua nchini jana alfajiri akitokea nchini kwao Brazil ametoa kauli hiyo kabla ya kuanza kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Simba imepangwa kundi C ikiwa na timu ya Horoya ya Guinea, Vipers ya Uganda na Raja Casablanca ya Morocco.
Kocha huyo raia wa Brazil, amepanga kuhakikisha kikosi hicho kinachoundwa na mastaa kama Jean Baleke, Ismael Sawadogo na wengineo wanapambana kuhakikisha Simba inarudisha makombe ambayo wameyapoteza msimu uliopita.
Akizungumza na Championi Jumatano, Robertinho alisema kuwa, kuna umuhimu kubwa kwake kuona wachezaji wake wanajituma kwa kucheza soka la kasi ili kuweza kuendana na wapinzani wao wa katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo malengo yao ni kufika nusu fainali.
“Wachezaji na timu kwa ujumla wanatambua ukubwa wa michuano ya ligi ya mabingwa hasa katika hatua ambayo imefikia lakini kwa bahati nzuri hakuna kati yetu ndani ya timu ambaye hajui ukubwa wa michuano hii kutokana na uzoefu wao kucheza msimu uliopita.
“Nadhani tunapaswa kuzingatia wachezaji waongeze juhudi za kujituma na kuhakikisha soka ambalo tunacheza litakuwa na kasi kwa kuweza kushambulia wakati wote kwa sababu wapinzani ambao tunaweza kukutana nao lakini itatusadia kuona tunafikia malengo kulingana na ubora wa wachezaji ambao tunapo nao,” alisema Robertinho.
Stori na Ibrahim Mussa