

Mbunge wa Kibaha Mjini, Slyvestry Koka (kulia) akijiandaa kunawa mikono ili kujikinga na ugonjwa hatari wa Corona (COVID-19) kabla ya kukabidhi mizinga hiyo ya nyuki.
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini, Slyvestry Koka, amekabidhi Mizinga 10 ya nyuki yenye thamani ya Shilingi Milioni 1.5 kwa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilya ya Kibaha mjini kwa ajili ya mradi wa ufugaji wa nyuki.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, katika Ofisi za CCM Kibaha mjini, Mbunge Koka aliipongeza jumuiya hiyo kwa kupata mwenyekiti mwenye maono makubwa ya kuiendeleza jumuiya hiyo kwa kuitafutia miradi mbalimbali.
“Niwapongeze Jumuiya ya Wazazi Kibaha Mjini kwa kupata Mwenyekiti Shunda ambaye anajitambua, mbunifu na Mchakarikaji katika kutaka kuacha alama kwa muda aliopo madarakani katika utawala Wake;
“Ninamfahamu tangia akiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Forest lililopo kata ya Kongowe, mengi nilishirikiana naye, tulijenga kwa pamoja shule ya msingi na sekondari ya Mwambisi lakini hata kuifufua zahanati ya Mwambisi iliyokuwa haifanyi kazi kwa muda mlefu” alisema Koka.
Aidha mbunge Koka, alisema kwa hamasa ya maendeleo ya Jumuiya ya Wazazi imempelekea Yeye Kama Mwakilishi katika Jimbo hilo la Kibaha kutoa mizinga 10 kwa ajili ya kuchagiza na kuendeleza mradi wa ufugaji wa nyuki ambao baada ya uvunaji wa asali utaipatia jumuiya hiyo kipato.
Akizungumza baada ya kupokea mizinga hiyo ya nyuki, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya CCM, Edwin Shunda, alimshukuru mbunge Koka kwa Kuipatia jumuiya hiyo mizinga na kusema awali walikuwa na mizinga 30 kwa kuongezewa mizinga 10 Sasa mizinga imefika 40.
“Kwa niaba ya Jumuiya ya Wazazi Kibaha mjini tunamshukuru mbunge kwa kutupatia mizinga 10 ya nyuki, tayari tuna mizinga 30 ambayo tumeshatundika kwenye shamba letu na kufikisha jumla 40” alisema Shunda.
Pia Shunda alitumia nafasi hiyo kuwashukuru meneja wa kanda wa wakala wa misitu Tanzania na mkurugenzi wa Idara ya Utafiti wa Miti Dawa Kutoka Muhimbili kwa Kuipatia jumuiya hiyo shamba Ekari 5 na maji kwa ajili ya ufugaji wa mradi wa nyuki utakaozalisha asali baada ya uvunaji na kuiletea fedha jumuiya hiyo.
Aidha katibu wa jumuiya hiyo Wilaya ya Kibaha mjini, Daima Utanga, alimshukuru Mbunge Koka kwa msaada huo wa mizinga 10 na akaahidi kutumia nguvu zake katika kuhakikisha mradi huo unafanikiwa kama ilivyolengwa.
NA: MWANDISHI WETU, KIBAHA

