The House of Favourite Newspapers

Mbunge Aliyehama Adai Chadema Waliratibu Mpango wa Lissu Kupigwa Risasi – Video

MBUNGE wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel amesema tukio la Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 jijini Dodoma ni mpango uliosukwa na Chadema na kutoa sharti kwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kuwa wakilitimiza atakuwa tayari kuthibitisha.

 

Dkt. Mollel ambaye alikuwa mbunge wa Chadema na baadaye kuhamia CCM ambako aligombea tena na kurejea bungeni akiwa amebadili chama, ameliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana Ijumaa kuwa yeye aliiba sampuli ambazo chama hicho kilimkataza kuzitumia.

 

Mbunge huyo amedai kuwa alipojaribu kuwasilisha sampuli hizo ili zipelekwe Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi alikataliwa na uongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani kwa kile alichodai walifahamu kuwa wangeumbuka.

 

“Mimi nilikuwa huko lakini nilikimbia kwa mipango yao, hata katika tukio la kushambuliwa Lissu mimi niliingia ndani kwenye uchunguzi na niliiba baadhi ya vitu lakini walikataa mapendekezo yangu,” alisema Mollel.

 

Hata hivyo, wabunge wa Chadema, Frank Mwakajoka (Tunduma) na Joseph Selasini (Rombo), kwa nyakati tofauti waliomba kutoa taarifa kuhusu hoja ya Mollel ambapo walimtaka mbunge huyo kuthibitisha kauli zake na kutovunja kiapo chake cha udaktari.

 

Katika majibu yake Dk Mollel alisema hawezi kuthibitisha hadi Chadema watakapomueleza fedha za ruzuku zinakwenda wapi na mpango waliotaka kuufanya kwa Zitto Kabwe (mbunge wa Kigoma Mjini) na marehemu Chacha Wangwe, walipotaka kugombea uenyekiti wa Chadema.

 

Lissu amekuwa mjadala kwa nyakati tofauti ndani ya Bunge wiki hii kutokana na kauli anazozitoa hivi karibuni katika ziara zake za ughaibuni.

Spika wa Bunge ameahidi kufanyia kazi hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Geita, Joseph ‘Msukuma’ Kasheku kuwa ofisi ya Bunge isitishe mshahara na stahiki za Lissu.

Comments are closed.