The House of Favourite Newspapers

Mbunge azua gumzo biashara ya mbwa

0

MBUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupitia Viti Maalum, Lucy Simon Magereli amezua gumzo la aina yake kwa jinsi anavyojituma kwa ujasiriamali ikiwemo biashara ya uuzaji wa mbwa wa kisasa.

Awali, gazeti hili lilielezwa na majirani wa mbunge huyo pamoja na watu wanaomfahamu kwamba ni mpambanaji ambaye mbali na ubunge, anajua kujituma kwenye ujasiriamali. “Wee, yaani huyu dada anajituma. Ni mjasiriamali ambaye kweli anajua kutumia fursa lakini kali zaidi inayomfanya azungumzwe kwa sasa hapa mtaani ni hii ya kuuza mbwa, imekuwa ya tofauti kidogo na nyingine,” Uwazi lilielezwa na mmoja wa majirani wa mbunge huyo.

Hivi karibuni, gazeti hili liliweka kambi nyumbani kwake Mji wa Wabunge-Kisasa, jijini Dodoma na kushuhudia mengi yenye kutoa funzo katika maisha. Uwazi lilishuhudia mbwa hao wa kisasa anaowafuga wakiwa kwenye banda lao maalum.

Mbunge huyo alieleza jinsi anavyowafuga kwa ajili ya biashara. “Ninao mbwa wa Kizungu ambao ninawafuga kwa ajili ya biashara, ni lazima maisha yasonge kwa namna yoyote, ubunge siyo ajira ya moja kwa moja, hiyo ni ridhaa ya wananchi, siku wakiamua wampe nafasi mwingine ajira ya uwakilishi inakoma hapo, ni lazima uwe na maisha mbadala kwa ajili ya malengo ya siku zijazo kwa watoto,” alisema Magereli.

Mbunge huyo hakusita kuzungumzia makazi yake ambayo pia kwa namna moja au nyingine, huweza kuwavutia wengine. “Kuhusu makazi, ninayo nyumba hapa Dodoma na Dar es Salaam, lakini nyumba si jambo la kusema, ingawa kwa kuwa uliniuliza, ni hivyo, ni jambo la kawaida,” alisema.

Akizungumzia maisha yake binafsi, alisema yeye ni mama wa familia. “Mimi ni mke na mama mwenye watoto wa kike ambao ni Maria na Marina, na ninawapenda sana wanangu, hivyo ninawalea katika misingi na maadili mema ili waje wajitegemee kwa maisha yao ya baadaye,” alisema.

Mbali na ufugaji wa mbwa hao, mbunge huyo anafuga kuku wa mayai, kuku wa nyama, pia anajihusisha na kilimo cha miti ya matunda, jambo ambalo humfanya awe na mambo mengi ya kufanya nje ya shughuli za kibunge katika kuwawakilisha wananchi.

Katika ujasiriamali wa ufugaji wa kuku, Magereli huuza mayai pamoja na nyama, hivyo kumuongezea kipato.

“Kuna maisha nje ya ubunge, unajua ubunge siyo kazi ya kudumu, hivyo ni lazima watu tuwe na akili ya kujiongeza kufanya mambo mengine kwa maana ya kujiongezea vipato na kusongesha maisha.

“Niliamua kujiongeza kwa kujishughulisha na ufugaji, na ufugaji pekee ambao niliona unaweza kuninufaisha ni ufugaji wa kuku wa mayai na wa nyama, maana ni kazi ambayo nilijifunza kutoka kwa mama yangu, nikiwa mdogo kabisa,” alisema Magereli na kuongeza;

“Ukiondoa ufugaji wa kuku, pia ninauza viungo mbalimbali kwa kuvitayarisha katika mazingira mazuri, kisha kuvifungasha kwenye vifungashio maalum na kuviuza kwenye maduka makubwa (super market). Ni maisha ya upambanaji, unajua ukiwa hai na mwenye afya njema, ni vizuri sana kujaribu mambo mengi, maisha ni kupambana,” alisema.

Pia mbunge huyo ambaye mwaka 2015 alijitosa kugombania jimbo la Kigamboni kupitia chama chake na kuambulia nafasi ya pili nyuma ya mgombea wa CCM, (Dk Faustine Ndugulile), anajihusisha na kilimo cha miti ya matunda ambapo alisema;

“Kilimo na ufugaji ni vitu vinavyoambatana, hivyo niliamua kuingia pia kwenye kilimo cha miti ya matunda, ambapo ninalo shamba kubwa kiasi lenye mchanganyiko wa miti mbalimbali kama maembe, machungwa, ndimu, limau na vitu vingine vingi, lengo ni kupambana na maisha kwa kufanya mambo kadha kama nilivyosema hapo awali, kwamba ni vyema kufanya mambo mabalimbali,” alisema mbunge huyo ambaye hana maneno mengi nje ya vitendo.

Leave A Reply