The House of Favourite Newspapers

Mbunge CCM Atishiwa Kuuawa

DAR: SIKU chache baada ya kuibua ufisadi mbele ya Rais John Magufuli, Mbunge Nkasi Kaskazini, Ali Keissy (CCM) amesema amekuwa akipata vitisho vya kuuawa pamoja na kunyang’anywa jimbo lake kutoka kwa baadhi ya ‘watu wasiojulikana’.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge huyo kufichua ubadhilifu wa zaidi ya Sh. bilioni nne katika jimbo hilo wakati Rais Magufuli alipofanya ziara mkoani Rukwa Oktoba 8, mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili, Keissy alisema licha ya kupokea vitisho hivyo, hatishiki na wala haogopi chochote kwa kuwa amenuia kwa dhati kumsaidia Rais Magufuli kutokomeza ufisadi na kuwaletea maendeleo wananchi wake.

 

Alisema vitisho hivyo amekuwa akivipokea kwa njia mbalimbali licha ya kwamba hajaripoti kokote lakini hatishiki kwa sababu anaamini hawawezi kumziba mdomo.

“Vitisho vipo, wananitishia hata kuniuwa kabisa, kuna watu wanasema huyu mbunge anatuzibia riziki kwa wakandarasi Namanyere, mtu mmoja anatupigia kelele bungeni kiasi hiki!

 

“Ila watu hao wanadhani Sumbawanga wamekuwa wapumbavu, eti wanahonga wapiga kura wangu ili watafute mbunge mwingine mwizi kama wao, hili jambo nilimwambia hata rais,” alisema.

Alisema uthubutu alionao katika kusema ukweli bila uoga unatokana na uaminifu alionao katika utendaji wake.

 

“Wabunge wachache ndio wanaojitokeza kufichua madudu, wengine waoga. Lakini hili jambo inategemea kwa sababu ukishachukua cha mtu huwezi kusema ukweli… kwa mfano mimi wamenifuata kutaka kunihonga nimekataa.

 

“Hata mimi ningekuwa nataka hela ningekuwa nahongwa, hakuna asiyependa hela lakini wananchi wamenichagua lazima niwatumikie kwa uweledi,” alisema.

Alisema Rais ndio amempa nguvu kwa sababu anaweza kuzungumza naye wakati wowote na kuchukua hatua.

 

”Rais mwenyewe ndio alinipa nguvu akaniambia kuwa jasiri kama kawaida usiogope, tena anachukua hatua nikimuambia,” alisema.

Aidha, aliwaomba wananchi, wabunge na watumishi wa serikali wamsaidie Rais kufichua uovu wowote unaotokea.

 

“Hii nchi yetu tajiri; kwa mfano, hii miradi miwili ya maji tu niliyozungumzia hapa ni bilioni 4.4 nimeokoa,” alisema.

Alisema ni dhahiri kuwa baadhi ya watumishi wa serikali wanashiriki kuiba fedha za serikali kwani mfanyabiashara au mkandarasi pekee hawezi kuiba.

 

UFISADI ALIOIBUA

Katika ziara hiyo ya Rais, mbunge huyo aliibua ufisadi katika mradi wa ujenzi wa bwawa la Mfili – Namanyere uliokuwa wa thamani ya Sh. milioni 730 lakini akadai haufiki hata thamani ya Sh. milioni 300.

 

Keissy pia aliibua mradi wa ujenzi wa chumba cha baridi kwa ajili ya kuhifadhia samaki huko Kirando uliogharimu Sh. milioni 356 lakini cha ajabu hauna uwezo wa kuhifadhi samaki na mkandarasi ametokomea na fedha zote.

 

Pia mradi wa umwagiliaji kwa wakulima wa mpunga huko Kirando wenye thamani ya Sh. bilioni 1.8 lakini alisema mpaka sasa hauwasaidii wakulima, ni mradi hewa na wakandarasi wamekimbia.

 

Aidha, alisema mradi wa maji wa Namanyere, mkandarasi alitaka kulipwa Sh bilioni 1.5 lakini baada ya Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kufanya uhakiki akabaini kwamba Sh. milioni 300 zimezidi. Hivyo akamtaka kumalizia kazi yake bila kulipwa hizo Sh. milioni 300, naye akakubali kufanya hivyo.

 

Mbunge huyo pia alipongezwa na Rais Magufuli kwa kuibua ufisadi huo kwa kuwa kila mara awapo bungeni hubainisha madudu yanayofanyika Rukwa kutokana na watendaji wasiowaaminifu kutozingatia maadili ya kazi zao.

 

“Ingekuwa inawezekana wabunge wanabadilishwa majimbo, basi ningesema uende Chato… sio kwamba kule hakuna mbunge mzuri, lakini wabunge wanaosema ukweli kama Keissy ni wachache.

“Niwaambie mna mbunge mzuri, mnamwona hapa anazungumza kwa dhati, ni wachache sana wa aina hii, amekuwa akiwakilisha mawazo ya wananchi,” alisema Rais Magufuli katika ziara hiyo.

Stori: Mwandishi Wetu, Amani

Comments are closed.