Mbunge Eric Shigongo Akabidhi Vifaa vya Michezo kwa Timu 22 za Shigongo Cup 2025
Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, ameonyesha dhamira yake ya kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana kwa kukabidhi rasmi vifaa vya michezo kwa timu 22 zitakazoshiriki mashindano ya Shigongo Cup, yatakayofanyika kuanzia Juni 24 hadi Julai 24, 2025.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Shigongo aliwataka viongozi wa timu kuhakikisha mashindano hayo yanasimamiwa kwa weledi, nidhamu na usawa, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kugundua, kuibua na kukuza vipaji vya vijana katika michezo.
“Michezo ni ajira, ni afya na ni njia mojawapo ya kuwaunganisha wananchi wetu. Tushirikiane kuitumia kama chombo cha maendeleo,” alisema Shigongo.
Katika kuongeza hamasa ya mashindano hayo, Shigongo alitangaza zawadi nono kwa washindi:
Mshindi wa kwanza: Ng’ombe watatu
Mshindi wa pili: Ng’ombe wawili
Mshindi wa tatu: Ng’ombe mmoja
Shigongo alisisitiza kuwa zawadi hizo ni sehemu ya kuwahamasisha vijana kuonesha uwezo wao kwa bidii na kujituma zaidi, huku akiahidi kuendelea kuwekeza katika sekta ya michezo ili kuleta mabadiliko chanya kijamii na kiuchumi.
Mashindano ya Shigongo Cup yamekuwa yakifanyika kila mwaka na kupata umaarufu mkubwa katika wilaya ya Buchosa na maeneo ya jirani, yakitoa jukwaa la kukuza vipaji na kuimarisha mshikamano wa kijamii kupitia michezo.