The House of Favourite Newspapers

Mbunge Hamoud Jumaa: Kipaumbele Changu ni Afya, Huduma za Jamii

0
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa (kushoto) akiongea na muandishi wa Mtandao huu, Denis Mtima.

NA DENIS MTIMA | UWAZI| HABARI

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa amekuwa akifanya kazi  za kuwaletea maendeleo wapiga kura wake na wananchi wa jimbo lake kwa juhudi na maarifa na amesema kipaumbele chake ni kwenye huduma za afya na huduma za jamii.

Safu hii hivi karibuni iliwahi kuwa na mbunge huyo katika shughuli mbalimbali anazozifanya jimboni kwake, ambapo ilijionea alivyokuwa akihangaikia ujenzi wa uzio wa Kituo cha Afya Mlandizi, mkoani Pwani na pia ujenzi wa soko katika eneo hilo ambapo baadhi ya watu waliufananisha utendaji kazi wake na aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe. Ungana nasi kwenye mahojiano kati ya mwandishi wetu na mbunge huyo yaliyofanyika katika maeneo ya kazi jimboni mwake ili umsikie:

 Nesi wa Kituo cha Afya Mlandizi akieleza juhudi za mbunge Jumaa.

Swali: Tangu umechaguliwa ubunge, miradi gani ya maendeleo umewafanyia wananchi wako?

Jibu: Hivi tunapozungumza nipo katika ujenzi wa uzio wa Kituo cha Afya cha Mlandizi ambacho kinatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 200 na kikikamilika kitaondoa kero iliyodumu miaka mingi.

Swali: Unadhani mradi huo ukiisha utasaidia nini?

Mbunge Jumaa akisalimia wananchi wake (hawapo pichani).

Jibu: Kimsingi kero ya ukosefu wa uzio ni kubwa na inasababisha usumbufu kwa wagonjwa kutokana na watu kupita bila kufuata utaratibu pamoja na pikipiki kuingia ndani ya kituo kwa kupita popote bila kujali kwamba hapa kuna wagonjwa, wengine hawatakiwi kusumbuliwa kwa kelele. Hivyo, ujenzi huu ukikamilika utawawezesha wagonjwa, wauguzi na madaktari kuwa katika sehemu salama kutokana na adha walizokuwa wakizipata kutokana na watu waovu ambao wangeweza kuingia kwa urahisi na hadi sasa tumekwishatumia zaidi ya shilingi milioni 45 na ujenzi unaendelea.

…Akikagua kituo cha afya.

Swali: Nini lengo lenu hasa?

Jibu: Lengo letu ni kutekeleza moja ya ahadi ya Rais Dk. John Magufuli ya kujenga hospitali aliyoitoa wakati wa kampeni za urais mwaka juzi. Lakini pia lengo letu sisi viongozi wa hapa ni kufanya kituo chetu kipande hadhi ili kuwa hospitali ya wilaya japokuwa pia kutokana na sera inavyosema kituo hicho hakiwezi kuwa hospitali ya wilaya lakini tayari tumekwishapata kiwanja kingine ambacho nina imani tutajenga hospitali hiyo ya wilaya hapo baadaye kwa awamu nyingine.

Swali: Bila shaka katika shughuli hizo za kuwaletea wananchi maendeleo unakumbana na changamoto mbalimbali, je unaweza kuziainisha?

…Akisalimiana na waendesha bodaboda.

Jibu: Kweli, zipo changamoto nyingi katika kituo chetu hiki na miongoni mwa changamoto hizo ni ukosefu wa chumba cha upasuaji na kuhifadhia maiti, upungufu wa  watumishi wa afya, madaktari lakini yote hayo kutokana na juhudi zangu na nikishirikiana na wananchi wangu nina imani zitapungua.

…Akifanya mahojiano na Global TV Online.

Swali: Je, unaizungumziaje kauli mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu katika jimbo lako?

Jibu: Kauli hiyo inatufanya sisi wawakilishi wa wananchi tufanye kazi kwelikweli tofauti na mitindo ya kizamani na ndiyo maana unaniona nafanya kazi bila kujali muda. Kuna siku nafanya kazi hadi usiku ili kupunguza kero za wananchi wa jimbo langu.

 

Swali: Licha ya mradi wa uzio wa kituo cha afya, kuna mradi mwingine unaendelea hapa katika jimbo lako?

Jibu: Ndiyo, tuna mradi wa ujenzi wa soko la kisasa la Mlandizi ambao umekwishaanza ambao ukimalizika hakika wananchi wangu wataweza kunufaika na soko hilo kutokana na kero ya hivi sasa wanayoipata ikiwemo kukosekana kwa miundombinu salama ya soko hilo. Harakati za ujenzi wa soko hilo pamoja na uzio wa kituo cha afya unatokana na jitihada kubwa za wadau mbalimbali kuniunga mkono.

Swali: Unadhani wananchi wako wananufaika na miradi hiyo wakati inapojengwa?

Jibu: Wananufaika kwa sababu mafundi wanaojenga uzio huo ni vijana wa jimbo langu hivyo wamejipatia ajira ya muda na wananufaika na fedha za mradi ambazo kama wasingepewa kazi hawa vijana wangu, wangepata mafundi wengine kutoka nje ya jimbo langu, jambo ambalo sikulikubali.

Swali: Je kuna mradi mwingine licha ya hiyo miwili?

Jibu: Ndiyo, kuna mradi wa kujenga kituo cha polisi ambacho tunataka kiwe cha wilaya. Hiki natarajia kuanza ujenzi wake baada ya kukamilika kwa miradi hii miwili ya ujenzi wa kituo cha afya na soko.

Leave A Reply