The House of Favourite Newspapers

Mbunge Haule: Vijana tumeonesha siasa siyo mchezo mchafu

0

prof jayWiki iliyopita safu hii ilizungumza na Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Joseph Haule, maarufu kama Profesa J na kuzungumza naye mambo mbalimbali kuhusu siasa hapa nchini na akasema kwamba  kuchaguliwa vijana wengi kuwa wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumeonesha kuwa siasa siyo mchezo mchafu. Kwa nini amesema hivyo? Fuatana nasi katika makala haya:

Kuna dhana kwamba siasa ni mchezo mchafu, wewe uliyeingia katika siasa unaweza kusema nini kuhusu usemi huo?

Jibu: Kwanza kabisa mimi nasema siasa siyo mchezo mchafu na ndiyo maana vijana wengi safari hii wamefanikiwa kuchaguliwa kwa ridhaa ya wananchi na kuwa wabunge. Zamani watu walikuwa na dhana kwamba ili uchaguliwe kuwa mbunge ni lazima utoe rushwa, lakini safari hii, yaani katika uchaguzi wa mwaka jana, hilo halikuwepo. Wengi waliotoa rushwa kama wapo, walipigwa chini ndiyo maana umeona vijana wengi wamechaguliwa kuwa wabunge. Mimi nasema nimekopeshwa kura na wananchi na nitawalipa maendeleo. Kilosa kuna kero kubwa ya mafuriko, ninaiomba serikali kuona hili kwani kuna tatizo la madaraja kushindwa kuhimili maji.

Kuna dhana kwamba  wabunge wanapoitwa waheshimiwa hufurahia utukufu huo, nini maoni yako kuhusu hilo?

Jibu: Kwanza mimi sipendi kabisa kuitwa mheshimiwa na badala yake napenda watu waniite mtumishi kwa sababu wamenichagua kuwakilisha Jimbo la Mikumi ili niwe mtumishi wao. Kwa hiyo mimi kifupi sipendi niitwe mheshimiwa kama wenzangu wanavyopenda kuitwa.

Unaposema hupendi kuitwa mheshimiwa, kwa nini uliamua kugombea ubunge? Je, si kweli kwamba ulikuwa ukiutaka uheshimiwa?

Jibu: Kusema kweli sikuwa na mawazo ya kuingia kwenye siasa. Nilikataa kuwa mwanasiasa lakini wananchi wangu wa Mikumi wakanijia na kuniambia , Profesa Ingia katika siasa na utaweza kutuwakilisha. Nilitafakari sana ombi lao, lakini yupo mtu mwingine akaungana na wananchi wa Mikumi kunishawishi kuingia kwenye siasa.

Mtu gani huyo aliyekushawishi?

Jibu: Ni Sugu au Mr 2 (Joseph Mbilinyi), Mbunge wa Mbeya Mjini, ndiye aliyenishawishi kuingia kwenye ubunge. Aliniambia nina uwezo wa kuwa Mbunge wa Jimbo la Mikumi.

Ulipoambiwa na Sugu, uliamua bila kuwa na mikakati ya ushindi?

Jibu: Hapana, baada ya kuombwa na wananchi wangu, Sugu ilikuwa kama amepigilia msumari. Tuliweka mikakati na wananchi na mbinu nyingine za ushindi alinipa Sugu kwa sababu alikuwa ameshakuwa na uzoefu nami niliamini kwa sababu nilikuwa nikimuona jinsi wapiga kura wake walivyompachika jina la utani kuwa ni Rais wa Mbeya.

Kwa siku chache ulizokalia kiti cha ubunge umebaini mambo gani mazito kwa wananchi wako?

Jibu: Kwanza kwa sababu  kazi yenyewe ndiyo naianza, jambo la kwanza nilitaka kujua changamoto za wapiga kura wangu. Nimepita kata 15 na vitongoji 109 kuwasikiliza, katika ziara hiyo nimejifunza mengi, nilikuta changamoto kubwa ni maji, elimu, miundombinu ya barabara  pamoja na ajira, nitaendelea kuwatumikia wananchi wangu kwa sababu wao ndiyo wamenituma Dodoma, mimi kuwa mwanamuziki haitanizuia kuwawakilisha wananchi… nitaendelea kuwa mwanamuziki na huwenda nikafanya muziki ule wa juu zaidi kwa sababu nategemea kukutana na watu wa juu zaidi. Nashukuru baadhi ya sehemu niliomba maji serikalini nikapata. Lakini pia  ilikuwa nafasi yangu ya kujifunza siasa, hali iliyonifanya kwa kipindi hicho cha zaidi ya miezi  minane nishindwe kufanya muziki ambayo ni fani yangu.

Una vision au maono gani kuhusu mambo ya kisiasa?

Jibu: Baada ya kuingia katika siasa naona naweza kusonga mbele zaidi. Sasa najiona kuwa naweza hata kuwa rais. Ndiyo, inawezekana. Kuna watu wanatafuta vyeo vya kupewa yaani kuteuliwa, lakini mimi siko huko ndiyo maana nasema naweza kuwa rais wa nchi huko mbele ya safari, hakuna ajabu. Kuna usemi unasema aliye juu mfuate huko huko.

Kuna madai kuwa wengi wenu bungeni hamjui Kiingereza, unazungumziaje hilo?

Jibu: Kutokujua Kiingereza siyo dhambi. Hii sijui Kiingereza, Kiingereza ni kushoboka tu. Viongozi wengi mbona tunaona wanakuja hapa Tanzania hawajui Kiingereza.

Tumeshuhudia bungeni wapinzani mkitoka nje ya ukumbi wa bunge, huoni kuwa mnawanyima wapiga kura wenu uwakilishi waliowatuma?

Jibu: Bungeni kunaongozwa na sheria na kanuni. Kazi ya wabunge ni kuisimamia serikali lakini sasa imekuwa kinyume, serikali inalibana Bunge na sasa limekuwa butu. Hakuna maana ya kukaa bungeni ukiwa umezibwa mdomo.

Unawaambia nini wapiga kura wako wa Jimbo la Mikumi?

Jibu: Nawashukuru sana wananchi wa Mikumi kwa kuniamini na kunipa dhamana hii kubwa, Watanzania wameniamini kwa sababu ya upeo mkubwa ambao Mungu amenipa, naamini sana katika umoja na mshikamano na ndiyo maana nimekuwa nasisitiza hata katika kampeni zangu, lazima tushikamane watu wote wa vyama vyote na hata wasio na vyama ili kuikomboa Mikumi yetu.

Profesor Jay Anena Haya kwa Mashabiki Wake wa Hip Hop Singeli


Profesor Jay “Mazuri na Mabaya ya Serikali ya Magufuli Niliyoyaona ni Haya Hapa’

Binti wa Miaka 19 Aliye Tembea na Wake za Watu Ndiye Huyu Hapa-Part I

PT 2- Binti wa Miaka 19 Aliye Tembea na Wake za Watu Ndiye Huyu Hapa-Part I

Mzungu Dar Afumwa Live Akilawitiwa na Vijana 3, O.F.M Yanyaka Tukio Zima

Leave A Reply