Mhamasishaji huyo amewaeleza wanachuo hao kuwa kila binadamu ana nafasi yake ya kufanikiwa na kwamba kinachotakiwa ni kujiamini na kuukataa mfumo unaowagandamiza hasa vijana na kuwanyima fursa ya kufanya maamuzi yao kwa uhuru.
“Naomba mnisikilize kwa makini, kijana uliyepo hapa leo na unayenisikiliza, una uwezo wa kufanya jambo kubwa na ukaacha alama siku ukiondoka duniani. Usisikilize watu wanachosema kuhusu wewe, ni Mungu tu aliyekuumba na kukupulizia uhai ndiye anafahamu makusudi ya kukuleta duniani na ukaacha alama hapa duniani.
“Amini kwamba unaweza kufanya jambo leo likabadili maisha yako na kukuondoa katika umasikini. Mimi familia yangu ilidharauliwa, niliitwa maskini, madaso na mjinga, nikaamini kwamba ni mjinga kweli, nikafeli darasa la saba na wala Sikwenda sekondari, lakini leo hii aliyeitwa mjinga ndiye ameshika hapa maiki. Ningeaamini maneno yao nisingekuwa Shigongo mnayeniona hapa,” alisisitiza.