MBUZI HAPEWI NYAMA

HAYA tena shoga kama nakuona vile unavyojiuliza inakuwaje gari lina sofa lakini si za mbao! Haloooo eeeeeh! Weee zubaa tu wakati zipu ina meno na haiwezi kupigwa mswaki, wereeee reeeee! Shoga tangu lini mkono wa mwenziyo ukajikunia? 

 

Unaringia shepu feki unasahau kama ukioga lazima uivue uweke pembeni, jamaaani! Wananiambia ohh Anti Naa siku hizi umezidi kuwa na mdomo, nikikufunda ndiyo waniita nina mdomo? Shuuutuuuuu!

 

Shoga hebu tuingie kwenye mada iliyonifanya leo hii niwe na wewe kwenye kona hii! Najua wengine itawachoma kama jua la mchana au pasi lakini ndiyo hivyo kitu kikishaingia kwenye koromeo sharti ukimeze, upo nyonyo?

 

Leo nipo na wale mama wa nyumbani na wengine wa maofisini ambao kutwa wanashindwa hata kuthamini dada wa kazi kutwa kuhamishia lawama kwao, akitenda mema wala huona ila akikosea basi utasema hadi nyumba ya tatu watajua, jamaaaani!

 

Hakuna mtu wa kumthamini katika dunia ya leo kama dada wa kazi, muwekee mazingira mazuri, sawa hatukatai kila binadamu ana mapungufu yake kutokana na alipokulia lakini unaweza kumrekebisha, siyo kavunja chombo basi unataka kwenda naye sawa mwisho wa mwezi!

Nikisemaga shoga huwa namaanisha, kuna mwingine anasoma hapa tangu mwaka jana hajampa binti wa kazi pesa yake, kutwa kumdanganya na nguo za msimu mara ohhh nilikununulia Krismasi mara ohh Pasaka hii itakuwa zamu ya wazazi wako nitawatumia, mara ohh nakutunzia hadi siku ukienda kuwasilimia ndugu zako, shuuuuutuuu!

 

Shoga hivi, anavyokulelea watoto wako huoni thamani yake, unavyomuachia anapika chakula cha nyumba nzima hadi cha mumeo humuoni ana thamani? Anavyohangaika na kuwasha jiko kwa kupuliza wakati mwingine anashinda juani akifua nguo bado huoni thamani yake?

 

Ifike mahali basi tumpe heshima zake huyu dada wa kazi, kama mimi dada wangu wa kazi kwa sasa anasomea cherehani, akimaliza namnunulia anaenda kwao kujiendeleza kwa maana hiyo nimeshampatia mtaji, na hapo wazazi wake nawatumia pesa na yeye sijawahi kumvusha pesa yake hata mwezi mmoja!

Shoga mbuzi hapewi nyama, kama unamthamini dada huyu basi huwezi kumgeuza mbuzi kusema utampa nyama ale wakati hali! Kwa leo nisiwe muongeaji sanaaaa, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri zaidi ya hii. Ni mimi Shangingi Mstaafu Anti Naa!

Loading...

Toa comment