The House of Favourite Newspapers

Mbwa 300 Kukutwa Nyumba Ya Serikali Dar… Giza Nene Latanda

GIZA limeendelea kutanda kufuatia mbwa wapatao 300 na paka kadhaa kukutwa hivi karibuni ndani ya nyumba ya serikali eneo la Oysterbey Mtaa wa Mawenzi Kitalu namba 823, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke ambayo ndiyo mmiliki wa nyumba hiyo, Lusubilo Mwakabibi, na viongozi wengine wa kamati ya ulinzi na usalama hivi karibuni walivamia kwenye nyumba hiyo na idadi hiyo kubwa ya mbwa sambamba na paka wote wakiwa wamefungiwa kwenye banda maalumu.

Habari hiyo ambayo ilienea kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii bado imeacha maswali kuhusu matumizi ya wanyama hao.

Watu wengi kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakijadiliana ni vipi nyumba hiyo ya serikali ya kisasa iliweza kuhifadhi wanyama hao bila kujulikana matumizi yake.

“Inawezekana wanachinjwa na kuwalisha wananchi kwa njia haramu, maana haiwezekani mtu afuge mbwa 300; kila siku awalishe bila kumuingizia fedha,” aliandika mwananchi mmoja kwenye ukurasa wa Instagram.

Hata hivyo, serikali baada ya kuvamia nyumba hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke, Lusubilo Mwakabibi, ilisema watu walikuwa wakiishi humo na kwamba ndiyo wanaohisiwa kufuga wanyama hao.

Waliokuwata katika nyumba hiyo waliojitambulisha kama mameneja wanajulikana kwa jina moja moja la Ngowi na Miriam.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mwakabibi licha ya nyumba hiyo kumilikiwa kihalali na Manispaa ya Temeke, imeelezwa kwamba imeuzwa kinyemela kwa raia mmoja wa kigeni jambo ambalo serikali inalifuatilia kwa karibu.

Aidha, baada ya habari hiyo ya mbwa kutoka na ukimya kuendelea kutawala mwandishi wetu alilazimika kuwatafuta baadhi ya viongozi wa serikali wilayani Temeke ili kujua nini kinaendelea kuhusu sakata hilo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Sophia Mjema alipotafutwa kwa njia ya simu, mara kadhaa simu yake iliita bila kupokelewa huku Mkurugenzi Mwakabibi simu yake ikionekana kutumika kila wakati.

Katika jitihada za kutafuta majibu ya habari hiyo ambayo bado yako gizani mwandishi wetu alimtafuta Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo ambaye alikiri kulifahamu jambo hilo na kuongeza kuwa:

“Tumeshamuita huyo mmiliki, tumemhoji na kumkabidhi kwa vyombo vya dola ili kuendelea na uchunguzi zaidi,” alisema Chaurembo na kuongeza kuwa jina lake hatalitaja kwa kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi.

Meya huyo alipoulizwa kuhusu madhumuni ya mbwa hao na paka kufugwa kwa wingi katika nyumba hiyo ya serikali alisema: “Hayo sasa tuviachie vyombo vya ulinzi na usalama vikijua ukweli vitatuambia.”

Awali wakati wa uvamizi katika nyumba hivyo mmoja wa vijana aliyekutwa mahali walipohifadhiwa wanyama hao alisema wamekuwa wakiwakusanya mbwa kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwahifadhi.

STORI: ELVAN STAMBULI

Comments are closed.