MBWEMBWE NDOA YA DIAMOND, TANASHA YAMKUTA YA WEMA, ZARI

DAR ES SALAAM: Mwanadada Tanasha Donna Barbieri Okech ‘Zahara Zaire’ kutoka Kenya ambaye siku za hivi karibuni aliingia kwenye penzi la ghafla na msanii wa muziki Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kisha kutangaziwa ndoa, yamemkuta yale yaliyowakuta mastaa waliowahi kutoka na mwanamuziki huyo, Zarina Hassan ‘Zari’ na Wema Sepetu, Risasi Mchanganyiko linakudadavulia ishu nzima.

 

KUHUSU AHADI YA NDOA

Siku chache baada ya Tanasha na Diamond kuingia kwenye dimbwi la mahaba, Diamond alitangaza kumuoa mrembo huyo haraka iwezekanavyo huku akiitaja Februari 14, mwaka huu (Siku ya Wapendanao) kuwa ndiyo siku ya kuandika historia kwenye maisha yake.

 

Ahadi hiyo ya ndoa ilikwenda sambamba na mbwembwe kibao za kuipa promo huku Tanasha ambaye ni Mtangazaji wa Redio NRG ya jijini Mombasa akifunguka kuwa, kwa bahati aliyoipata ya kuolewa na staa huyo, sherehe ya harusi yake itachukua siku nne nchini Kenya na kwa upande wa Bongo anamuachia mumewe mtarajiwa.

YALEYALE YA WEMA, ZARI

Wakati mashabiki wa mastaa hao wakiisubiri kwa hamu ndoa hiyo, Diamond juzikati aliibuka na kueleza kuwa, kutokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wake, ameahirisha tukio hilo mpaka pale itakapotangazwa tena.

 

Diamond aliweka wazi kuwa, moja ya sababu zilizomfanya aahirishe ndoa hiyo ni kukosekana kwa mastaa wakubwa wa muziki duniani akiwemo William Leonard Roberts ‘Ricky Ross’ na wengine aliofanya nao kolabo ambao alitarajia wawepo lakini hawatakuwa na nafasi siku hiyo.

 

“Ni kweli nilitarajia kufunga ndoa Siku ya Valentine’s (Februari 14) lakini kuna watu ambao hawatakuwepo hivyo nimesogeza mbele. Wanatarajiwa kuwepo akina Rick Ross na wengine niliofanya nao kolabo sasa kwa kuwa hawatakuwepo, nimeahirisha mpaka hapo baadaye,” alisema Diamond.

 

Kufuatia maelezo hayo, baadhi ya watu wanaofuatilia kwa karibu maisha ya kimapenzi ya mwanamuziki huyo walisema kuwa, kinachomtokea Tanasha ndicho kilichowatokea Zari na Wema walipokuwa kwenye uhusiano na staa huyo kwani nao waliwahi kuahidiwa ndoa lakini haikutokea.

 

Akikomenti kwenye ukurasa wa Instagram wa Diamond baada ya kuona taarifa ya kuahirishwa kwa ndoa hiyo, mdau mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Ziggy J alisema: “Kinachompata Tanasha sasa hivi ndiyo kilekile kilichowapata Zari na Wema. Mtakumbuka wakati Diamond yuko na Wema alitangaza kumuoa tena kwa mbwembwe sana, akamvisha hadi pete ya uchumba pale Maisha Club enzi zile lakini baadaye wakamwagana.

“Achana na Wema, Diamond huyuhuyu alipokuwa na Zari ishu ya ndoa ilionekana wazi ingechukua nafasi. Tambo zikawepo nyingi sana, jamaa akajitapa kuchukua jiko jumlajumla, tena akaahidi pia ndoa yao itatikisa Afrika lakini kiko wapi?

 

“Leo hii tena baada ya kuwa tunasubiria kwa hamu ndoa iliyopangwa kufanyika mwezi Februari tunaambiwa imeahirishwa eti kisa akina Rick Ross hawatakuwepo, kweli inaingia akilini hii? Hapa napo sidhani kama kuna ndoa. Mtasikia tu….”

 

WENGI WALISHAHISI CHANGA LA MACHO

Hata kabla Diamond hajatangaza kuwa ameahirisha ndoa yake, wapo baadhi ya watu ambao walishaanza kueleza kuwa, wanahisi ishu ya ndoa ya Tanasha na Mond ni changa la macho kutokana na jinsi penzi lao lilivyochipukia.

 

Wapo waliokwenda mbele zaidi na kudai kuwa, penzi la wawili hao ilikuwa ni kiki kwa ajili ya shoo ya Tamasha la Wasafi Festival lililofanyika hivi karibuni Mombasa, Kenya na kwamba wakati wowote wanaweza kumwagana.

MAKONDA AMTUPIA MONDI DONGO

Kufuatia maelezo ya kwamba ndoa hiyo imeahirishwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni Mlezi wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Paul Makonda amemrushia dongo kiaina Diamond kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram hivi:

 

“Sipati picha waleeeeeeeeee waliotuacha wanavyokutazama. Mmoja eti anasema unaigiza. Nakuomba MC Pilipili umsaidie na Diamond kwani yeye kila tarehe ikikaribia anasogeza mbele, ona sasa anamsubiri Rick Ross aje, sasa sijui ni harusi au tamasha.”

 

NDOA IPO, HAIPO?

Kufuatia haya yanayoibuka na kusemwa kila siku, wengi wamekuwa wakijiuliza swali moja tu kwamba, ndoa ya Diamond ipo au haipo? Jibu sahihi la swali hili liko ndani ya moyo wa Diamond mwenyewe hivyo sisi tuvute subira, mbivu na mbichi zitajulikana.

Loading...

Toa comment