The House of Favourite Newspapers

MC Pilipili Amuomba Mondi V-8 la Tanasha

0

NI Jumamosi nyingine mpenzi msomaji tunakutana kwenye My Style. Hapa tunaweza kuzijua staili mbalimbali za maisha ya msanii akiwa nyumbani. Leo tunaye mchekeshaji, Emmanuel Mathias ‘MC Pilipili’. Ungana naye;

 

My Style: Ratiba yako kwa siku ukiamka huwa ikoje?

Pilipili: Cha kwanza huwa nafanya ibada na kumkabidhi Mungu siku, pia baada ya hapo napanga mambo nitakayoyafanya siku hiyo kisha baada ya kupanga, natafuta yale magumumagumu ndio naanza nayo.

My Style: Tunafahamu kuwa unajishughulisha na mambo mengi sana; U-Mc, uchekeshaji, uchungaji, utangazaji, mume na mambo mengine mengi, vipi unawezaje kupangilia muda wako kufanya mambo yote hayo tena kwa ubora uleule?

 

Pilipili: Kwenye Biblia pia imeandikwa kwamba, ‘Nayaweza mambo yote katika Yeye anitiaye nguvu’ kwa hiyo, mambo yote ninayofanya nayaona magumu lakini ukiwa umetambua kitu ambacho Mungu amekiweka ndani yako, mara nyingi kunakuwa na nguvu ya ziada ambayo inakusukuma kufanya vitu unavyovipenda, hivyo unajikuta unavifanya bila kuchoka.

Lakini pia vitu vyote ninavyofanya vina asilimia kama 80 za ucheshi, hivyo kila ninachofanya watu lazima wacheke kidogo, hivyo inakuwa inanirahisishia hata mimi.

 

My Style: Tunafahamu kwamba wewe ni mshauri wa mambo kadhaa; ikiwemo na uhusiano, vipi kwa upande wako huwa ukiwa na tatizo kwenye ndoa yako, nani unamfuata kama mshauri wako?

Pilipili: Kwanza lazima watu watambue kwamba, linapotokea jambo, watu wa kwanza kabisa kulitatua ni nyie wenyewe, ikishindikana ndipo mnawashirikisha watu mnao waamini.

 

Kwa upande wangu, nikiwa na tatizo kwenye ndoa yangu, mara nyingi naenda kwa watumishi wa Mungu, sanasana huwa naanza na wasimamizi na mapatroni wangu, na marafiki kama walezi mtu kama Antoni Luvanda.

My Style: Nimekuwa nikifuatilia sana shughuli unazofanya na mara nyingi unafanya vizuri, lakini pia huwa unaitendea haki sekta ya mavazi, nani ambaye huwa anakuvalisha? Au huwa unabuni mwenyewe mavazi yako?

Pilipili: Nina watu kadhaa ambao huwa wananivalisha; mtu kama Kitupe, pia kuna mtu anaitwa Wensi, lakini wale huwa wananishonea ila mke wangu ndio huwa anaamua nivae nini. Kwa ufupi, yeye ndiye anayenipangia mavazi yangu.

 

My Style: Ukiwa na msongo wa mawazo, huwa unafanya nini ili kuweka akili yako sawa?

Pilipili: Kitu cha kwanza huwa ni maombi, kwa sababu Biblia inasema; njooni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kuelemewa na mizigo.

Halafu jambo la pili kama imetokea nipo mbali, basi narudi nyumbani kwa sababu nyumbani ndio sehemu inayonipa furaha zaidi.

My Style: Kati ya saa, pete, simu na cheni, ni kitu gani ambacho huwezi ukatoka bila kuwa nacho?

Pilipili: (Anacheka) pete, yaani siwezi kutoka bila pete aisee.

 

My Style: Mfano ikatokea siku umesahau simu yako nyumbani na mkeo yupo, utarudi kuichukua?

Pilipili: (Anacheka tena) aaaah nitarudi kuifuata, au kama mazingira ya mimi kurudi ni magumu, basi nitamtuma hata bodaboda, kwa sababu mimi napenda sana kuchezea simu yangu.

Lakini pia kitu ambacho huwa nasahau sana mpaka nachanganyikiwa ni charger na mara nyingi nikipotezaga basi lazima ninunue nyingine.

 

My Style: Starehe yako kubwa ni nini?

Pilipili: Starehe yangu kubwa ni kuangalia movie na tamthiliya ya Selina na Pete, maana zimebadilisha mpaka ratiba yangu ya kurudi nyumbani.

My Style: Ukitulia nyumbani na familia yako, huwa unapenda kufanya nini?

 

Pilipili: Nikiwa nyumbani na mke wangu, napenda sana kula halafu nitatafuta mtumishi yeyote wa Mungu nitamsikiliza kisha baada ya hapo nitaangalia komedi.

My Style: Kitu gani ambacho kinakuvutia sana kwa mkeo?

Pilipili: Navutiwa sana na yeye kumjua Mungu, lakini mbali na yote ni mwanamke mzuri na mwenye mvuto, hivyo namshukuru Mungu kwa hilo.

My Style: Unaweza kutoka na mkeo akiwa hana make up?

 

Pilipili: Ndio, naweza kutoka naye akiwa hana make up usoni, kwa sababu ni msichana mzuri sana hata akiwa hana make up.

My Style: Unapenda kutoka naye akiwa katika muonekano upi wa mavazi?

Pilipili: Unajua mke wangu akivaa sketi ni balaa, gauni ni hatari, suruali ni hatari zaidi, hivyo avae vyovyote mimi huwa napenda.

My Style: Aina gani ya nguo ukivaa unajiona upo comfortable zaidi?

 

Pilipili: Mimi napenda sana nikivaa casual kama jinzi na t-shirt.

My Style: Unatembelea gari gani na gari ya ndoto yako ni ipi?

Pilipili: Natembelea BMW lakini gari ya ndoto yangu ni V-8 kama ya Diamond ile (Anacheka), dah naipenda sana. Naomba basi Mondi anipe ile V-8 aliyompa Tanasha maana ndio dream car yangu kwa sababu Tanasha alisema hakuondoka nayo aliiacha hapa nchini. Hivyo Simba kaipaki tu, na najua Diamond hana roho mbaya, atanipa tu.

 

My Style: Kiasi gani cha pesa huwezi kukitoa kumlipia mkeo kufanya make up?

Pilipili: Mimi naweza kutoa kiasi chochote kile, kwa sababu ni mke wangu na furaha yangu pia.

My Style: Tunafahamu kwamba Corona imeathiri sana utendaji kazi wako, labda unafanya nini kipindi hiki ili kuhakikisha unazidi kuingiza kipato?

 

Pilipili: Nashukuru Mungu kwamba mambo yanaendelea japo si sana, lakini mke wangu hivi karibuni alikuja na wazo la kufanya biashara na tukaamua kuanza kuuza samaki sato fresh na wazuri kabisa, hivyo tunafanya delivery pia.

My Style: Jambo la mwisho kwa mashabiki wako.

Pilipili: Nawapenda sana na ndio maana nimeanza utaratibu wa kufanya Quarantine Comedy Show kila Jumapili kwenye Instagram yangu, hivyo kila Jumapili huwa nakuwa live nikifurahi na mashabiki zangu. Nawapenda!

MAKALA: MEMORISE RICHARD

Leave A Reply