McCarthy Ashinda Uspika wa Bunge la Congress la Marekani kwa Mbinde
Baada ya vuta nikuvute iliyochukua muda wa siku nne na kusababisha uchaguzi wa Spika wa Bunge la Congress nchini Marekani urudiwe mara 15 baada ya mshindi kutopatikana, hatimaye Kevin McCarthy, ameibuka mshindi katika raundi ya 15 ya uchaguzi huo uliovunja rekodi.
McCarthy wa chama cha Republican, alikuwa akichuana vikali na mgombea mwenzake, Hakeem Jeffries wa chama cha Democrat, anachotokea spika aliyemaliza muda wake, Nancy Pelosi.
McCarthy ametangazwa kuwa Spika wa 118 wa Bunge la Congress, akipata kura 216 huku Hakeem akipata kura 214 na kumfanya atangazwe kuwa mshindi kwa tofauti ya kura nne pekee.
Mzunguko wa mwisho wa kupiga kura, umefanyika usiku wa Januari 6, 2023 siku ambayo ni kumbukumbu ya tukio la kuvamiwa kwa Bunge la Capitol, mwaka 2021 baada ya Donald Trump kutangazwa kuangushwa kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hiyo na mpinzani wake, Joe Biden ambaye ndiye rais wa sasa wa Marekani.
Taarifa zinaeleza kwamba, Mc Carthy alikuwa akiungwa mkono na Trump, huku akipingwa vikali na baadhi ya wanachama wa chama chake cha Republican, akidaiwa kuwa hatoshi kuvaa viatu vya uspika wa bunge hilo ambalo lina ushawishi mkubwa katika siasa za Marekani.