The House of Favourite Newspapers

‘Mchawi’ wa Diamond, Ali Kiba, Q-Chillah 2016 Huyu Hapa

 


mbwana-mtuliya-d-bass-1 

Mwaka 2016 unaelekea ukingoni lakini kuna vionjo vipya vimeingia kwenye tasnia ya Bongo Fleva! Hebu sikiliza kwa makini wimbo wa Utanipenda wa Diamond unapoanza! Unasikia ‘melody’ ya kifaa kama kinanda kinachosikika? Njoo kwenye wimbo wa Aje wa Ali Kiba, pale unapoanza tu kuna kifaa kinasikika kama gitaa flani hivi, unakisikia?

Hamia kwenye wimbo wa Mkungu wa Ndizi wa Q- Chillah akiwa na TID, unakisikia hicho kifaa kinachosikika hapo mwanzo? Umeshaelewa nataka kuzungumzia nini? Basi kwa taarifa yako, kifaa hicho chenye sauti tamu masikioni, kinachoupa muziki ladha ya kipekee, kinaitwa Ganun.

Kilikuwa kikitumiwa sana na wanamuziki wa zamani, hasa kutoka mwambao wa Pwani kuupa muziki ladha ya kipekee lakini sasa, kinarudi upya kwa kasi na safari hii, kimeingia kwenye Bongo Fleva.

Ipo wazi kwamba ukizisikiliza nyimbo hizo, utagundua kuna kitu fulani tofauti ambacho huwezi kukipata sehemu nyingine, sauti ya kifaa hiki ni kama uchawi ambao unakulazimisha uendelee kusikiliza wimbo fulani mara kwa mara.

mbwana-mtuliya-d-bass-2

Mbwana Mtuliya ‘D-Bass’.

Lakini je, unamjua mtu aliyepo nyuma ya uchawi huo? Showbiz Xtra, imefanya mahojiano na msanii pekee upande wa Tanzania Bara anayepiga kifaa hicho, ambaye ndiye aliyetumika kupika nyimbo nilizozitaja hapo juu; si mwingine bali ni Mbwana Mtuliya ‘D-Bass’ ambaye hivi sasa amekuwa lulu kwa wanamuziki wengi.

Kwa nini aliamua kujifunza kupiga chombo hicho?

D-Bass: Unajua chombo hiki si maarufu sana na ndiyo maana nikaamua kujifunza kwa sababu nilijua wazi watu wengi hawakifahamu na nilitaka kuwa wa tofauti kabisa  kwani watu wengine unakuta kila mmoja anajua kupiga gitaa au hata ngoma sasa kunakuwa hakuna tofauti na wengine na hii ni kama zawadi ya maisha yangu.

Alijifunzia wapi kupiga Ganun?

D-Bass: Nilijifunza kupiga chombo hiki Zanzibar, ambapo nilisoma chuo kwa muda wa miaka mitano  na nilipoelewa kabisa nilimaliza chuo ambapo sasa hivi naweza kukutumia vizuri sana.

Kuna mwanamuziki yoyote anayeweza kukitumia chombo hiki?

D-Bass: Kwa Tanzania Bara ni mimi peke yangu lakini kwa Zanzibar wapo wazee wa zamani wanaoweza kukitumia chombo hiki ambapo hata mimi ujuzi wa kupiga Ganun nimeupata Zanzibar na kama ningeenda kusomea nje ya nchi ingekuwa ni Uarabuni kwa sababu ndio chombo chao.

Kwa nini haonekani kwenye video za wanamuziki alizopiga chombo hicho?

D-Bass: Sikutaka kabisa mwanzo kuonekana  kwenye video ya nyimbo za mwanamuziki yoyote kwa sababu nilitaka kazi yangu ijulikane kwanza na siyo sura yangu hivyo baada ya kufanya hivyo wanamuziki wengi wakawa wananitafuta lakini hawakuwa wanajua sura yangu.

Aliwezaje kumshawishi Diamond kumpigia kwenye wimbo wake?

D-Bass: Kwanza nilitumia nguvu nyingi sana kwa sababu nilipata namba yake nikawa nampigia mara nyingi na kumtumia kazi zangu sikuwa napata majibu, sasa kuna siku nilishasahau kabisa ndipo aliponitafuta  yeye mwenyewe akasema nataka tufanye kazi ndiyo nikampigia kwenye ngoma yake ya Utanipenda.

mbwana-mtuliya-d-bass-3

Ganun yake ameinunulia hapa hapa Bongo?

D-Bass: Hapana hii ninayotumia nilipewa zawadi na mwalimu wangu kwa sababu ni mwanafunzi ambaye nilikuwa natumia muda mwingi sana kwa vitendo darasani na usikivu wa hali ya juu hivyo alinipenda na kunipa zawadi hiyo.

Ana chombo kingine anaweza kupiga?

D-Bass: Ndio mimi napiga sana Bass Guiter, na ndio maana hata jina langu nilijiita hivyo  na bado nina kiu ya kujifunza sana vitu vingine vingi pia ni vizuri kujua vitu tofautitofauti  na muziki mzuri ni wa vionjo asilia.

Kuna faida yoyote ameshaipata?

D-Bass: Hapana sio kubwa ila kiu yangu ya kufanya na wanamuziki wakubwa imekamilika na kutambua thamani ya chombo hiki kwenye muziki wao hapo sasa ndio naweza kusema nasaka faida ya kimaslahi.

Anakitumia chombo hicho hata jukwaani?

D-Bass: Ndio mara nyingi kwenye matamasha makubwa ya ndani na nje ya nchi ndio nakipigaga na ndio kazi yangu na watu wanakuwa wanahisia kali ninapokipiga.

halotel-strip-1-1

MZEE WA MIAKA 76 ALEYETANAGAZA KUTAFUTA MKE “FULL EXLUSIVE INTERVIEW”

Comments are closed.