The House of Favourite Newspapers

Mchekeshaji Erick; Mtaalam wa Wali Maharage


KWA UFUPI: Katika Makala ya MpakaHome kupitia Gazeti la Risasi Jumamosi, Mchekeshaji Sobogani Zabron Erick Kisauti wa Vituko Show amesema ni mtaalam wa wali maharage

 

MAKALA: Na Imelda Mtema | RISASI JUMAMOSI| MPAKA HOME

MAMBO vipi mpenzi msomaji wangu wa safu hii tamu ya Mpaka Home, kazi yangu kubwa kwako wewe msomaji ni kukupa kitu kilicho bora zaidi na ndio maana kila wiki tunawaletea maisha ya mastaa mbalimbali Bongo nje ya sanaa wanayoifanya.

Wiki hii safu hii ilikuwa mitaa ya Tabata-Mawenzi, jijini Dar ambapo ilimtembelea mchekeshaji Sobogani Zabron ‘Erick Kisauti’ wa Vituko Show iliyokuwa inaruka katika Luninga ya Channel Ten, twende pamoja:

Mpaka Home: Erick bila kupoteza wakati, tueleze maisha ya kawaida na ya ustaa kuna tofauti gani kwa upande wako?

Erick: Tofauti ni kubwa sana. Ya kawaida unaweza kufanya vitu vingi bila macho ya watu lakini sasa hivi inakulazimu kutumia gharama nyingi sana kuanzia usafiri, mavazi na kila kitu ili tu uishi kistaa.

Mpaka Home: Nini unapenda kukifanya  unapokuwa nyumbani?

Erick: Mimi rafiki yangu mkubwa ni TV, napenda sana kuangalia tamthilia mbalimbali za kuweza kujifunza vitu kutokana na kazi ya sanaa ambayo naifanya.

Mpaka Home: Vipi kuhusu upande wa mapishi, unapendelea nini? Unaingia mwenyewe jikoni au kuna mtu anakusaidia kazi hiyo?

Erick: Mimi ni mwanaume ambaye napenda sana kupika chakula, kikubwa ni wali na maharage na sitaki kujifanya kidume kwamba siwezi kuingia jikoni.

Mpaka Home: Vipi kuhusu chakula cha mama ntilie, ulishawahi kula au unakula mpaka sasa?

Erick: Yaani hicho ndio chakula chetu sisi na si unajua mara nyingi tuko mitaani na ninaridhika kabisa maana siwezi sema naweza kwenda mahoteli ya gharama kula.

Mpaka Home: Vipi umeshaoa? Una watoto?

Erick: Nimeshaoa na nina mtoto mmoja wa kike.

Mpaka Home: Kutokana na kazi yako najua watoto wengi wa kike wanakusumbua vipi mkeo anasemaje halimpi shida hilo?

Erick: Hapana kwanza niko naye muda mrefu sana na yeye ndio ananipa moyo siku zote.

Mpaka Home: Hivi sauti yako kuwa nyembamba, ndivyo ulivyo au huwa unajifanyisha unapokuwa unaigiza?

Erick: Mimi kama unavyoniona hapa nazungumza kawaida na hii sauti alinifundisha mwalimu wangu wa sanaa Joli Taxi, na watu naona wanaipenda sana.

Mpaka Home: Kwa nini umesuka nywele?

Erick: Hii ni staili yangu niliamua kutoka hivyo kunogesha sanaa yangu, ninaipenda sana.

Mpaka Home: Je unapenda mwanao afuate nyayo zako?

Erick: Hapana kabisa sitaki huku ni kugumu mno bora afanye kitu kingine kabisa.

Mpaka Home: Hapa unapoishi umepanga au ni nyumba yako mwenyewe?

Erick: Nimepanga, Mungu akipenda nami huko mbeleni nitakuwa na nyumba yangu.

Mpaka Home: Nakushukuru sana Erick.

Erick: Karibu sana.

Comments are closed.