The House of Favourite Newspapers

Mchizi Mox Akataa Kuitwa Mkongwe, Awataja Wakongwe

Taikuni Ally ‘Mchizi Mox’

MWANAMUZIKI Taikuni Ally ‘Mchizi Mox’ ni miongoni mwa wanamuziki wenye majina makubwa kwenye gemu la Muziki wa Bongo Fleva hasa kwenye upande wa Hip Hop.

Aliibuka mwaka 2000, akiwa na Kundi la Wateule lililokuwa linaundwa na yeye mwenyewe, Jumanne Mchopanga ‘Jay Moe’ pamoja na Jaffari Ally ‘Jaffarai’, ambapo wimbo wao wa kwanza uliowatoa unaitwa Watu Kibao walioufanya mwaka 2000.

Miaka minne baadaye (2004), Mchizi Mox ndipo alifanya ngoma akiwa mwanamuziki solo, wimbo uliitwa Mambo Vipi na ulipokelewa vizuri kwenye gemu.

Nyimbo nyingine alizofanya akiwa peke yake ni pamoja na Demu Wangu aliofanya na marehemu Albert Magwea, pamoja na Chupa Nyingine. Akiwa na Wateule, wamefanya ngoma nyingi pia ambazo ni Msela, Nipende Nichukie na wimbo wao wa mwisho kutoa ni Vile Vile waliotoa mwaka 2011 wakiwa wamemshirikisha Solo Thang, huku video yake wakifanyia Afrika Kusini na Ireland alikokuwa anaishi Solo Thang!

Kimya kirefu kimepita Mox hasikiki hewani kwani wimbo wa mwisho alitoa 2015, unaitwa Simba Bado Anawinda.

Kwa nini yupo kimya na mengine mengi, huyu hapa Risasi linamleta kwako. TWEND’ ZETU!

Risasi: Mox vipi mzee, kimya sana tatizo nini?

Mox: Niliamua kujipa mapumziko si unajua tena gemu nimefanya muda mrefu sana.

Risasi: Mapumziko yamekuwa marefu sana, lini yatakwisha?

Mox: Nategemea kurudi mwezi Julai. Nipo ninakamilisha kazi yangu mpya hasa kwenye upande wa video, kwa hiyo nitarudi.

Risasi: Utakuwa peke yako au kuna mwanamuziki umemshirikisha?

Mox: Nitakuwa peke yangu. Unajua mwanamuziki ambaye tulikuwa tunaelewana sana alikuwa ni marehemu Albert Magwea, sasa ameshafariki. Wengine ni Wateule, sasa nisipofanya na hao nitakuwa peke yangu.

Risasi: Kwa muda ambao upo mapumziko nini ambacho umekisoma kwenye gemu?

Mox: Ni siri yangu kwa sababu hiyo ndiyo silaha yangu ambayo nitarejea nayo. Lakini kuna jambo linanikera sana.

Risasi: Jambo gani tena?

Mox: Media imeshindwa ‘ku-handle’ muziki, imebaki kufuatilia maisha ya wanamuziki, ambayo unakuta ni mambo ya ajabuajabu, ndiyo maana wanamuziki kama sisi ambao tupo muda mrefu kwenye gemu hawatupi nafasi kwa sababu hatupendi mafagio yasiyo na maana kwenye maisha yetu binafsi.

Risasi: Lakini kumbuka mwanamuziki ni ‘package’ kubwa, mashabiki wenu wanapenda kufahamu mengi kutoka kwenu na media inatii kiu ya mashabiki. Huoni hilo?

Mox: Sawa, lakini kwa nini mambo mazuri tukifanya hatusapotiwi?

Risasi: Kama suala lipi ambalo media haikusapoti?

Mox: Kwa mfano kwa sasa mimi ni balozi wa Taasisi ya GUTz (Get Up Tanzania), ambapo tunakwenda vijijini na kuhamasisha watu wafanye vipimo vya Ukimwi. Mambo kama haya hayazungumzwi lakini Mox akilewa akazima ndiyo media mtatoa.

Risasi: Ni wajibu wako pia kuzitafuta media, ili zifahamu una nini na wakusapoti, kama ambavyo media inakutafuta kukusapoti ingawa upo kimya.

Mox: Haina shida mzee.

Risasi: Kuhusu Wateule vipi, ndiyo kundi limeshavunjika hivyo au?

Mox: Kundi lipo kwa sababu Wateule ni watu na watu wenyewe wapo hai. Nipo mimi ninafanya mambo yangu, Jay Moe anafanya yake na hata Jaffarai. Tunashindwa kuwa pamoja na kufanya kazi ya pamoja kwa sababu kwanza hatuna menejimenti lakini pia kila mtu ana majukumu ya kifamilia.

Risasi: Hivi kwa sasa ushaoa na kuwa na familia?

Mox: Hapana. Sijaoa ila nina mtoto mmoja. Mungu akisaidia ipo siku nitaoa.

Risasi: Kuna kipande cha video kimesambaa mitandaoni hivi karibuni ukisema kwamba hutaki kuitwa mkongwe, kwa nini?

Mox: Mimi siyo mkongwe. Nimetoka kimuziki mwaka 2000 tu alafu mtu ananiita mkongwe na kina mzee King Kiki na Zahir Zorro waitwe kina nani mana wameanza muziki miaka ya 1970 huko?

Risasi: Lakini tukizungumzia Bongo Fleva wewe ni mkongwe, kwa maana wakati unatoka ni mwanzoni kabisa wakati aina hii ya muziki inaanza kushika kasi, utakataaje kuitwa mkongwe kwenye gemu la Bongo Fleva?

Mox: Haijalishi. Muziki una ‘generation’ wala hauna mkongwe. Kuna ‘generation’ ya kina mzee King Kiki wapewe sapoti yao, ‘generation’ ya kwangu tupewe sapoti yetu na hata ya wadogo zangu nao wapewe sapoti yao.

Risasi: Umesomeka Mox, tulainishe mazungumzo, play-list ya ngoma unazosikiliza kwa sasa ni ipi?

Mox: Napenda Kwa Ngalu ya Harmonize, wimbo mpya wa Ali Kiba- Mvumo wa Radi, wimbo wa Kundi la The Mafik, napenda nyimbo za Young Killer na Nikki Mbishi.

Risasi: Pamoja sana, jambo lolote la mwisho?

Mox: Nawapenda mashabiki zangu na nikirudi nitawafurahisha sana.

MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.