MCHUMBA WA BEN POL ATOBOA SIRI KUPUNGUA KILO 47

KISTAAJABU ya Wema Isaac Sepetu utaona ya Anerlisa Muigai! Mwishoni mwa mwaka jana, Wema alipukutika kiasi cha kushtua wengi ambapo wapo waliodai alikuwa amefanya operesheni ya kukatwa utumbo mkubwa ambapo alipungua mwili na kuwa kama binti wa umri wa chini ya miaka 18 aliposhirikia Shindano la Miss Tanzania mwaka 2016.

 

Taarifa ikufikie kuwa mshtuko kama huo uliwahi kuwatokea watu baada ya mchumba wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Benard Paul ‘Ben Pol’, Anerlisa, raia wa Kenya. Anerlisa alipotea machoni kwa watu akiwa bongenyanya, lakini miezi tisa baadaye akaibuka akiwa kimbaumbau.

 

Anerlisa kwa sasa anazua mijadala Bongo baada ya kumnasa Ben Pol na kuendeleza wimbi la mastaa wa kiume Bongo kutekwa kimapenzi na warembo kutoka Kenya. Ni baada ya Aminah Khaleaf kuolewa na Alikiba na Tanasha Donna kuwa na Diamond Platnumz.

Baada ya kupukutika, Anerlisa alibanwa aeleze alichokifanya hadi akapungua kwani watu wengi walitamani kuwa kama yeye.

Kuna watu wamekuwa wakihangaika kupunguza miili kwa kwenda ‘gym’, kukimbia, dayati, dozi za mitishamba, kukatwa utumbo mkubwa na mengine kama hayo ambao walihitaji kupata ‘siri ya urembo’.

Ilikuwa mwaka 2016 ambapo Anerlisa ilibidi atoboe siri yake kwani alionekana kama aliyetoka uzeeni na kurudi ujanani ambapo ndani ya miezi hiyo alifanikiwa kupungua uzito kwa kilo 47.

Wafuasi wake walitaka awape ‘tips’ za nini alichokifanya hadi akapata mafanikio hayo makubwa;

Katika mahojiano yake na vyombo mbalimbali vya habari, Anerlisa mwenye ukwasi mkubwa akitajwa kumiliki kiwanda cha maji ya kunywa alifunguka;

“Nadhani nimekuwa nikijaribu kuwajibu baadhi ya watu kwa upole.

 

MAZOEZI

“Katika miezi miwili ya mwanzo nilipotaka kupungua nilikuwa ninafanya mazoezi mazito kwa muda wa saa moja kila siku. Mazoezi haya yalijumuisha kutembea na mazoezi ya mwili ya kujikunja (yoga).

“Miezi minne iliyofuata nilifanya mafunzo ya matumizi ya viungo kwa msaada wa mwanajeshi mstaafu. Hapa ndipo nilipopoteza uzito mkubwa wa kilo 30 kwa miezi hiyo minne kisha kilo 17 miezi mingine iliyofuata.

“Niliendelea na mafunzo hayo ambapo huwa ninatumia saa moja kila siku kwa ajili ya mazoezi.

 

DAYATI

“Mimi mwenyewe niliamua kusitisha kabisa matumizi ya sukari. Situmii vitu vya sukari kabisa. Niliamua kuwa ninapikia mafuta ya olive ambayo hayanenepeshi tofauti na mafuta mengine. Napendelea vyakula vya kuchemsha au kukausha kama nyama. Huwa ninapima kiwango cha ‘kabohaidreti’ kwa kijiko cha chai. Pia ninakunywa maji mengi hadi lita tano kwa siku. Napendelea vyakula vya protini kama maharage kwani ukila kidogo tu hushibisha kwa muda mrefu bila madhara ya kusababisha unene.

“Nakula sana mboga aina ya sukuma wiki na spinachi kwa wingi kwa ajili ya kupata vitamini.

 

NJAA

“Kama ukifanya mazoezi sana na ukawa unaona matokeo, basi niamini mimi, kitu pekee utakachokuwa unatamani ni msosi. Ndicho kitakachokuwa kimetawala akili yako. Hakikisha ‘unaji-control’ kula tena kupita kiasi kwa ajili ya njaa utakayokuwa nayo.

 

TUMBO

“Tumbo ndilo lilikuwa la kwanza kupotea kwa sababu wakati nikiwa na mwili mkubwa ndilo lilikuwa linaninyima raha, hivyo nilifanya sana mazoezi ya tumbo na ninaendelea nayo.

MICHIRIZI

“Baada ya kupungua mwili, mtu unabaki na michirizi, lakini hilo lina matibabu mengi mno hivyo unachagua tu utumie dawa gani za ngozi kwa maelekezo ya daktari.

“Naamini kwa maelezo yangu hayo, nimejibu swali lililokuwa likiulizwa na wengi na naamini kama na wewe unateswa na unene, utaanza kutafuta mabadiliko.

 

“Hakikisha unazungukwa na watu wenye lengo kama lako la kupungua, siyo unataka kupungua halafu muda wote upo na watu wanene, wasioona umuhimu wa kupungua kwani hao watakukatisha tamaa ili ufanane nao.

“Jishawishi mwenyewe kwa kuzingatia jinsi unavyokula zaidi. Kwangu mimi nilichukia nilipowasikia watu wakijadili unene wangu, hao walinishawishi kujituma sana ili kuondokana na unene.

“Mafanikio ndiyo njia bora kabisa ya kulipiza kisasi, lakini kumbuka unafanya hayo yote kwa ajili yako na kwa afya yako.”

 

MAKALA: Sifael Paul na mtandao

Dakika 8 za Nandy Jukwaa la Uzinduzi wa Coke Studio 2019

Toa comment