The House of Favourite Newspapers

MCHUMBA WA GODZILLA AIBUA UTATA

SIKU chache baada ya kifo cha msanii wa Hip Hop, Golden Mbunda ‘Godzilla, mrembo aliyejinasibu kuwa ndiye alikuwa mchumba wa marehemu, Isabela Mpanda ‘Bella’ ameibua utata wa aina yake kutokana na kauli zake.  

 

Bella alianza kukinukisha saa chache tu baada ya msanii huyo kufariki dunia usiku wa Februari 12, mwaka huu nyumbani kwao, Mbezi- Salasala jijini Dar baada ya kuugua kwa muda mfupi ugonjwa wa Malaria huku pia akisumbuliwa na tatizo la presha pamoja na sukari.

 

Baada ya tukio hilo, Bella alianza kukinukisha mitandaoni kwa kujitambulisha kwamba yeye ndiye mpenzi wa mwisho wa marehemu na kwamba alikuwa akipika na kupakua na Godzilla hadi dakika za mwisho za uhai wake.

FULL KUJINASIBU

Bella alienda mbali zaidi kwa kutupia picha mbalimbali za yeye na Godzilla na kuonesha jinsi gani ameguswa na msiba huo wa mtu wake wa karibu huku akiudhihirishia umma wa Watanzania kwa kuonesha shati ambalo inaonekana walikuwa wakivaliana na marehemu.

 

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Bella aliunganisha picha mbili tofauti; moja ya kwake na nyingine ya Godzilla ambayo inaonesha wamevaa shati hilo la rangi ya bluu katika nyakati tofauti huku akisindikiza na ujumbe mfupi uliosomeka: “Hili shati Zila…” ulisomeka ujumbe huo ulioambatana na ‘emoji’ za vilio.

 

UTATA WAIBUKA

Baada ya Bella kusema hayo, Risasi Jumamosi lilizungumza na rafiki wa karibu na Bella ambaye alionesha kushtushwa na kitendo cha Bella kujitambulisha kwamba alikuwa na uhusiano na marehemu wakati miezi michache iliyopita alichumbiwa na mwanaume mwingine aitwaye John aliyejaliwa kuzaa naye mtoto mmoja.

 

“Kwa kweli hapa ndiyo ninashindwa kumuelewa shoga yangu, maana nimejiuliza anakuwaje tena na uhusiano na Godzilla wakati na yeye alikuwa ameshavalishwa pete na mipango ya kuelekea kwenye ndoa ilikuwa imeshashika kasi,” alisema rafiki huyo aliyeomba hifadhi ya jina na kuongeza:

 

“Kama mnakumbuka, jamaa huyo alizaa naye na akamvisha pete kabisa na mambo yakawa moto kila mtu akaamini anaoa sasa sijui imekuwaje maana hivi ghafla tu anasema alikuwa na uhusiano na Godzilla halafu hata sisi marafiki zake hatujui?”

 

TAARIFA ZA KIFO…

Kama hiyo haitoshi, Bella alitengeneza utata mwingine kupitia kauli yake ambayo aliitoa kwenye vyombo vya habari pindi alipohojiwa kwamba mpenzi wake huyo alifariki akiwa katika Hospitali ya Lugalo tofauti na alichokisema dada wa marehemu, Joyce Mbunda. Bella kwa kujiamini, bila hofu yoyote akiwa msibani, alikaririwa akisema alikuwa na marehemu siku ya tukio na kwamba anachofahamu yeye ni kwamba umauti ulimkuta akiwa Lugalo.

 

DADA’KE GODZILLA…

Kwa upande wake Joyce, yeye alisema baada ya kumuuguza kwa takriban siku tatu, Godzilla alifariki akiwa mikononi mwake nyumbani kwao.

RISASI LAMBANA BELLA

Ili kujiridhisha zaidi, juzi Alhamisi, Risasi Jumamosi lilimvutia waya Isabella na kumbana maswali kuhusiana na utata huo ambao umejitokeza ambapo hakutaka kuzungumza kuhusu utata wa taarifa za kifo, zaidi ya kusisitiza kwamba yeye alikuwa mchumba halali wa marehemu na kwamba alishaachana na mwanaume aliyemchumbia takriban miezi mitano iliyopita.

 

Bella alisema, baada ya kuachana naye, aliamua kurejea kwa Godzilla ambaye aliwahi kuwa mpenzi wake kabla ya kuchumbiwa. “Niliachana na baba mtoto wangu nikaamua kurudi kwa mpenzi wangu wa siku nyingi ambaye ni Godzilla hivyo ndivyo ninavyoweza kusema kwa sasa, naomba uniache maana nipo kwenye majonzi,” alisema Bella.

 

Risasi Jumamosi lilijaribu kuwatafuta ndugu wa karibu wa Godzilla msibani lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa matunda hadi tunakwenda mitamboni kutokana na wahusika kuwa kwenye wakati mgumu wa kuzungumza.

 

TUJIKUMBUSHE

Godzilla ambaye alisifika kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuimba mashairi ya papo kwa papo (free style), alizaliwa mkoani Morogoro mwaka 1988 ambapo alianza rasmi shughuli za muziki mwaka 2007. Miongoni mwa nyimbo ambazo zilimweka kwenye ramani ya mastaa kutoka Bongo ni pamoja na Salasala, Lakuchumpa na Nataka Mkwanja.

VIDEO: WAZIRI WA JK AFUNGA NDOA NA KABINTI KABICHI

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.