The House of Favourite Newspapers

Mchungaji adaiwa kukamatwa na madawa na kunyongwa China

0

Makongoro OGING’ na Issa Mnally, UWAZI

DAR ES SALAAM: Hatari! Jeshi la Polisi Kikosi cha Kuzuia na Kudhibiti Madawa ya Kulevya Tanzania limesema linafuatilia kwa kina madai kuwa, aliyekuwa Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la Breakthrough Assemblies of God lenye makao yake makuu Boko jijini Dar (jina linahifadhiwa kwa sasa), amekamatwa na madawa hayo ‘unga’ nchini China na kunyongwa.

Akizungumza na Uwazi, Jumamosi iliyopita, kamanda wa kikosi hicho, Godfrey Nzowa alisema baada ya kupokea taarifa hizo, anawasiliana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) na ubalozi wa Tanzania nchini China ili kuona kama kuna ukweli wowote.

“Nimepokea taarifa hiyo, nitakachofanya mimi, nitawasiliana na ubalozi wetu nchini China sambamba na Interpol ili kuona kama kuna ukweli wowote,” alisema Nzowa.

MSEMAJI WA JESHI LA POLISI
Advera Bulimba (pichani) ni msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania ambapo kwa upande wake, akizungumzia madai hayo alisema:

“Nimechukua jina lote la huyo mchungaji, nafuatilia suala hilo kwa karibu sana ili nione kama kuna ukweli wowote.”

HABARI ZA MCHUNGAJI HUYO
Kwa mujibu wa chanzo chetu, mchungaji huyo na mkewe, walikamatwa wiki chache zilizopita wakiwa na unga aina ya cocaine ambao uzito wake na gharama za pesa hazijawa wazi.

Ilisemekana kuwa, mara baada ya kukamatwa, walifikishwa mahakamani na kupatikana na hatia ambapo walihukumiwa kunyongwa, lakini adhabu hiyo kwa mwanamke ilisitishwa baada ya kubainika kuwa ni mjamzito, hivyo mamlaka za China zinasubiri ajifungue, anyonyeshe kwa umri unaotakiwa ndipo anyongwe.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa kiongozi huyo wa kiroho aliacha kuhudumu katika kanisa hilo miezi sita iliyopita.

MCHUNGAJI KIONGOZI
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Gosbert Simtomvu alikataa kuthibitisha kuhusu madai hayo, lakini alikiri kusikia taarifa hizo ambazo ziliwaliza waumini wengi kwa vile mchungaji huyo alikuwa mwanafamilia.

“Kweli alikuwa mchungaji wangu hapa kanisani lakini aliondoka miezi sita iliyopita akasema anakwenda kuhudumu kwingine. Baada ya hapo sikupata taarifa zake hadi hivi karibuni ziliponifikia habari kwamba eti alinyongwa. Mimi sina uhakika lakini.

“Tupo katika maombi ya kumwombea kwa Mungu ili amlinde na taarifa hizo kama si za kweli,” alisema mchungaji huyo.

Leave A Reply