MCHUNGAJI mmoja na raia watatu wa Nigeria wamekuwa wakisota mahabusu jijini Dar, kwa zaidi ya miezi saba kwa madai ya kukutwa na madawa ya kulevya ‘unga’ aina ya heroin.
Mchungaji huyo ni Henry Ozoemana Ogwuanyi na wenzake, Onyebuchi Ogbu na Lucy Oding. Wote hao wanakabiliwa na kesi ya kukutwa na kilo 15.8 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Awali, Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya cha Polisi Tanzania, ACP Alhaj Kabaleke Salim, baada ya kuwakamata alizungumza na waandishi wa habari kuelezea sakata hilo kisha kuwafikisha mahakamani.
Hata hivyo, ufuatiliaji wa gazeti hili umebaini kuwa washitakiwa hao, wakiwa rumande baada ya kupanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, wameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini Tanzania (DPP) kukiri kosa la uhujumu uchumi linalowakabili.
Wakili wa Serikali, Elia Athanas aliieleza mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa washtakiwa hao wameandika barua kwa DPP kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri makosa yanayowakabili.
“Washtakiwa hao wameandika barua ya kukiri makosa yao, lakini DPP bado hajajibu barua hiyo. Ninaiomba mahakama ipange tarehe nyingine,” alisema Athanas. Baada ya maelezo hayo, wakili wa utetezi, Hassan Kiangio alidai kuwa suala la kuandika barua kwa washitakiwa hao isiwe kikwazo cha kutoendelea na kesi hiyo, akaomba upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi ili shauri hilo liende mbele.
Awali, akisoma hati ya mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi, Kakua alisema washitakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na shitaka moja la kukutwa na dawa za kulevya kinyume cha sheria.
Alisema washitakiwa hao walitenda kosa hilo Aprili 2, mwaka huu katika eneo la Msimbazi, Wilaya ya Ilala jijini Dar. Alidai siku hiyo ya tukio, Ogwuanyi na Ogbu walikutwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 15.8 kinyume cha sheria.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, Hakimu Shaidi alisema washitakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kutokana na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa Mahakama Kuu au kwa kibali maalum.
Tangu wakati huo, washitakiwa hao wamekuwa wakisota rumande kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana. Siku ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Kamanda Salim alisema; kukamatwa kwa mchungaji Ugwuanyi kulitokana na taarifa walizopewa na raia mwingine wa Lativia, Linda Mazule ambaye alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Aprili 17, mwaka huu akiwa na kilo 5.091 za heroin. Linda alimtaja mchungaji huyo kuwa ndiye aliyempa dawa hizo azisafirishe kwenda Poland.
Alisema kitengo chao kilipoendelea kumuhoji Linda, aliwaeleza kuwa alifika nchini Aprili 11, mwaka huu akiwa na mpenzi wake ambaye naye ni raia wa Lativia, Plavin aliyekuwa anatarajia kusafiri na dawa za kulevya Aprili 20, mwaka huu kwenda Poland.
“Baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, tulipata taarifa za siri za watuhumiwa wengine ambao walikuwa wakishirikiana kuuza na kusambaza dawa hizo za kulevya kuwa wapo jijini Dar,” alisema Kamanda Salim.
Salim alisema walifanya operesheni katika Jiji la Dar na viunga vyake ili kuwabaini wauzaji na wasambazaji hao kwa ushirikiano na vyombo vingine vya dola na taasisi za kiserikali zenye mamlaka ya kisheria.
Alisema Aprili 21, mwaka huu, majira ya saa 6:00 usiku, mkuu wa kitengo hicho alipokea taarifa kuwa watuhumiwa hao walikuwa maeneo ya Msimbazi-Kariakoo na walipofanya msako walifanikiwa kumkamata Plavin.
Katika uchunguzi wao, walibaini Plavin aliingia nchini na Linda aliyekamatwa Uwanja wa JNIA Aprili 17, mwaka huu na kuwa walikuwa wamepanga chumba kimoja katika hoteli moja (jina tunalo) iliyopo Kariakoo.
Kamanda Salim alisema baada ya kuhojiwa, Plavin alikiri kujihusisha na biashara haramu hiyo kwa kushirikiana na raia wawili wa Nigeria Ugwuanyi na Ogbu ambao walikuwa wamepanga nyumba namba tisa ghorofa ya nne katika mtaa wa Pemba uliopo Kariakoo.
Alisema Plavin aliwapeleka hadi kwa anayejiita Mchungaji Ugwuanyi na walipomkuta aliwapeleka hadi eneo alikopanga nyumba Mtaa wa Pemba na kuwaonesha chumba alichokuwa akiishi.
Kamanda huyo alisema baada ya kuingia ndani ya chumba chake, walimkuta Mnigeria Ogbu ambaye ni mtaalam wao wa kutambua dawa za kulevya.
Baada ya kufanya upekuzi katika nyumba hiyo, watuhumiwa walikutwa na kiroba kilichojazwa mchele, ndani yake kukiwa na pakiti 15 za heroin zenye uzito wa kilo 15.
“Tulipowahoji Ugwuanyi alidai yeye ni mchungaji na hata gari lake kaliandika mchungaji na Ogbu yeye ni mtaalam na kazi yake ni kujua kama ni dawa za kulevya na kama siyo anasema na anatambua ni aina gani ya dawa za kulevya hizo,” alisema Kamanda Salim.
Kamanda huyo alisema baada ya kuhojiwa, Ugwuanyi alidai kuwa yeye yupo nchini tangu mwaka 2017 akiwa kama mchungaji na pia akijihusisha na biashara hiyo
Comments are closed.