MCHUNGAJI AZUA BALA AGESTI

DAR ES SALAAM: Dunia ina mambo! Mchungaji na nabii aliyejulikana kwa jina la Stekamba Bin Mariam anayetoa huduma ya uponyaji kwa hisia ‘Meditation’ amezua balaa katika nyumba ya kulala wageni ‘gesti’, Amani limenasa tukio kamili.  

 

Mchungaji huyo alizua balaa hilo Jumatatu iliyopita maeneo ya Chanika, Dar baada ya kuvamia ndani ya gesti (jina linahifadhiwa) na kuanza kuwahubiria wateja. Katika maelezo yake mchungaji huyo alisema karama hiyo ya uchungaji na unabii alishushiwa na Mungu alipokuwa katika Milima ya Uluguru, Morogoro na kuanza kupewa maono mbalimbali na Mungu.

 

HAVAI VIATU

Cha kushangaza wakati akiendelea kutoa huduma hiyo mchungaji huyo alikuwa ‘peku’ yaani hajavaa viatu ambapo alieleza kuwa katika maisha yake hajawahi kuvaa viatu kwa sababu anaogopa kuikanyaga ardhi bila nidhamu. Mchungaji huyo ambaye alisema hana dini yoyote kati ya hizi za kidunia ikiwemo Ukristo wala Uislam na nyinginezo ambapo aliwaponda wanaojiita manabii hapa duniani huku wakitumia vitabu vya manabii wengine kufundishia wakati walitakiwa wawe na vya kwao.

 

“Nabii unatakiwa uwe na kitabu chako kitakatifu kwa ajili ya kuwafundisha watu neno la Mungu lakini nawashangaa hawa wanaojiita manabii kutumia maneno ya manabii wengine, sasa huo ndiyo unabii gani?” alihoji mchungaji huyo. Alisema, yeye tayari ana kitabu chake kitakatifu ambacho kitaingia kwenye kumbukumbu ya vitabu vitakatifu muda siyo mrefu.

 

Akiendelea kutoa neno, Mchungaji Stekamba ambaye alikuwa na baadhi ya wafuasi wake aliwasisitiza waliokuwa wakimsikiliza ndani ya gesti hiyo kwamba kama hawatawatii mama zao waliowaleta duniani basi hawawezi kuuona ufalme wa Mungu kwa kuwa mama ndiye Mungu wao wa duniani.

 

WATU WAMSHANGAA

Kutokana na mahubiri yake ya kuwahubiria watu waliopo gesti tu huku akiwa hajavaa viatu watu walijikuta wakipigwa na butwaa kwani hawakuwahi kuona mchungaji anayetangaza neno la Mungu kwa staili hiyo.

 

“Kweli siku za mwisho watajitokeza manabii wengi kama Biblia inavyosema tunatakiwa kuwa macho sana kuhusiana na hawa watu, sasa huyo mchungaji na nabii mahubiri yake na matendo anayoyafanya siyo yale tuliyoyazoea makanisani na misikitini tunakosali, ukweli amenishangaza sana,” alisema Esther ambaye ni mmoja wa wahudumu wa gesti hiyo.

 

Wahudumu mbalimbali wa gesti hiyo walimsikiliza na kukubali kuombewa na mchungaji huyo hasa wanawake (wanaoonekana pichani ukurasa wa mbele) ambao walimwambia shida yao ni kwamba wanataka waolewe na wanaume wa maana kwa sababu wamechoka kuishi bila wanaume.

Mchungaji huyo aliwaambia hilo ni jambo dogo sana ambapo aliwawekea mikono kichwani na kifimbo chake anachotembea nacho alichodai kina nguvu ya damu ya mwanamke mwanamwari na nguvu kubwa ya uponyaji.

 

Pamoja na kuwaombea, mchungaji huyo alitoa utabiri wa kifo chake kwamba kitasababishwa na mwanamke. Baada ya kumaliza kuhubiri na kuombea watu alianza kuagiza vinywaji vikali na kuanza kunywa, alipoulizwa kuhusu hilo alisema hata Mungu aliuumba mnazi na kuuwekea pombe juu yake na kusema alifanya hayo si kimakosa hivyo pombe haina shida, tatizo ni kuzidisha pamoja na matendo utakayofanya baada ya kulewa.

 

Aidha, siku za hivi karibuni aliibuka mchungaji mwingine aitwaye Nabii Tito ambaye mahubiri yake alihamasisha ulevi, kutembea na watumishi wa ndani jambo ambalo lilikuwa likiwashangaza wengi. Baada ya kusababisha matukio mengi alifikishwa mahakamani ambapo chombo hicho cha kutafsiri sheria kilimuona ana kasoro ya kiakili hivyo kuamuru apelekwe Hospitali ya Mirembe, Dodoma akatibiwe.

 

Katika kuonesha kuwa wimbi la wahubiri wa kila aina limeibuka, hivi karibuni mchungaji mwingine kutoka Afrika Kusini alidaiwa kusambaza video zikionesha kuwa amemfufua mfu jambo ambalo lilileta tafsiri tofauti miongoni mwa jamii.

 

Wengi waliotazama video hiyo waliitilia shaka na kusema huenda ni tukio la kutengenezwa kwa ajili ya kuwavutia watu, jambo ambalo liliilazimu Serikali ya Afrika Kusini kuamuru uchunguzi wa tukio hilo kufanywa haraka.

MHARIRI:

Ni vyema watu kuwa makini katika masuala yanayohusu imani ili kuepuka manabii wa uongo kama ilivyosema Biblia.

Stori: Richard Bukos, Amani

Toa comment