MCHUNGAJI AZUA TAFRANI KARIAKOO

DAR ES SALAAM: Ukisikia neno mchungaji amezua tafrani na kufunga mtaa mchana kweupe lazima utabaki na maswali mengi, imekuwaje kwani matukio kama haya ni nadra kuhusishwa wachungaji! 

 

Iko hivi; Mchungaji wa Kanisa la Emmaus Bible Church la Mbezi Luis jijini Dar, Daudi Mashimo amezua tafrani eneo la Kariakoo jijini Dar baada ya kumuokoa kijana mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja aliyekuwa akishambuliwa na wananchi kwa tuhuma za kutaka kuiba simu.

 

Kwa mujibu wa chanzo, tukio hilo lilijiri hivi karibuni ambapo kijana huyo alifika katika duka moja la kuuza simu katikati ya Kariakoo akiwa na muonekano ambao si rahisi kumgundua kama ni ‘mwizi’. “Haikuwa rahisi kumgundua kijana ambaye aliingia kwa lengo la kununua simu kwani alikuwa mtanashati yaani kama mwanafunzi wa chuo, mgongoni akiwa na kibegi cha kuwekea madaftari au kompyuta.

 

“Kilichomfanya anaswe ni pale alipojifanya anachagua simu lakini kumbe alichukua nyingine na kuweka mfukoni. Wauzaji pale walimshika na kuanza kumtembezea kichapo huku umati ukikusanyika na kufanya mtaa usipitike kwa muda kutokana na tafrani,” kilisema chanzo.

 

Baada ya kijana huyo kuendelea kupewa kichapo, Mchungaji Mashimo alitokea akiwa kama mpita njia na kuzua tafrani katikati ya watu kwa kuwakataza wasiendelee kumpiga.

 

“Licha ya kutokea mzozo na ubishi wa hapa na pale huku timbwili likitokea kama lote; mwishowe Mchungaji Mashimo alijitahidi kuwazuia wale raia wenye hasira kali kwa kuwaambia maneno ya Mungu kwamba yule kijana bado mdogo anaweza kubadilishwa kwa maombi siyo kipigo.

“Wale watu wakamuamini mchungaji na kumuacha aendelee kumkanya tabia ya wizi ambapo baadaye ya muda alimkokota na kumpeleka kusikojulikana,” kilisema chanzo ambacho kilifanikiwa pia kuchukua picha za tukio. Amani lilimtafuta Mchungaji Mashimo kujua alipoishia na kijana huyo na sababu hasa za kumtoa kwenye mikono ya raia wenye hasira kali.

 

“Ni kweli tukio hilo lilitokea Kariakoo na ilikuwa kama bahati wakati napita katika maduka nikifanya kazi yangu niliyotumwa na Mungu kuwaombea watu nikaona watu wengi wamemzunguka kijana huyo wengine wakimpiga na kumwambia maneno ya kuwa ni mwizi.

 

“Nilijaribu kuingilia kati japo haikuwa rahisi, nikawaomba wasiendelee kumpiga kijana yule kwani watu kama wale wanatakiwa kusamehewa na wanahitajika bado na Mungu hivyo wakanielewa na kutoka naye pale,” alisema Mchungaji Mashimo na kuongeza;

 

“Nilitoka naye moja kwa moja nikiwa nimemshika shati lake asiweze kuniponyoka na kwenda kumpeleka sehemu salama yaani kituo cha polisi pale Msimbazi,” alimaliza kusema Mchungaji Mashimo.

 

Mchungaji Mashimo ambaye pia hupenda kujiita Mchungaji wa Mitume na Manabii, ametokea kujizolea umaarufu kwa ghafla baada ya kuhusika katika kumtolea dhamana msanii Rutyfiya Abubakary maarufu kama ‘Amber Rutty’ baada ya kuwekwa mahabusu kwa tuhuma za kusambaza video yake chafu ya ulawiti.

Stori: Andrew Carlos, Amani
Toa comment