Mchungaji Bongo Aibuka Upasuaji  wa Kimiujiza

 

MCHUNGAJI Kiongozi wa Kanisa la Jerusalem lililopo Kitunda jijini Dar, Nabii James Nyakia ameibuka na upasuaji wa kimiujiza, RISASI Jumamosi linakupa habari kamili.

Habari za mchungaji huyo kufanya upasuaji kwa kutumia vidole zilifika kwenye dawati la gazeti na kuelezea jinsi watu wanavyopona kupitia miujiza hiyo.

 

“Huyu mchungaji amekuwa akiwapima watu kupitia viganja vyake vya mikono, yaani viganja vyake vinaku-scan mwili mzima kama kuna tatizo la uvimbe au magonjwa mengine mbalimbali anayaona.

 

“Ni muujiza kweli maana akishayaona magonjwa yanayokusumbua kama yanahitaji upasuaji basi anakufanyia kwa kutumia vidole vyake na kuna watu kibao wameshapona kupitia oparesheni yake,” kilisema chanzo ambacho kilidai ndugu yake alipona kupitia muujiza huo.

 

MCHUNGAJI ASAKWA

Ili kuujua undani wa habari hizo, RISASI Jumamosi lilimsaka mchungaji au Nabii Nyakia na kufanikiwa kufanya naye mahojiano ofisini kwake Sinza na kufafanua mengi kuhusiana na upasuaji wake kwa kutumia mikono.

 

Awali, mwandishi wetu alishuhudia vitanda viwili vilivyotandikwa mashuka meupe ndani ya ofisi yake na alipoulizwa alisema hivyo ni kwa ajili ya kuwapima wagonjwa pamoja na kuwafanyia upasuaji.

“Hivi vitanda ni maalumu kwa ajili ya kupimia wagonjwa na kuwafanyia oparesheni wale wenye matatizo ya uvimbe, ambao hawana uvimbe nawaombea na wengi wamepona,” alisema Nabii Nyakia.

 

ADAI NI KARAMA

Akizungumza Nabii Nyakia alisema huduma hiyo ya kupima ugonjwa kwa kutumia viganja vyake vya mikono pamoja na kufanya oparesheni kwa vidole ni karama aliyopewa na Mungu japo mtu wa kawaida hawezi kuamini.

 

Aliendelea kusema amekuwa akifanya huduma hiyo kwa watu wengi na waumini wake wanaposikia kwamba kesho watafanyiwa oparesheni wanafurahia maana wanaona ndiyo ukombozi wao.

 

“Hivi viganja vyangu vya mikono nikivipitisha juu ya mwili wa mtu naona kila ugonjwa au tatizo linalomsumbua, yapo mengine ambayo huwa nawaambia kabisa waende hospitali lakini mengine nawafanyia tiba mimi ndiyo maana umenikuta na koti la kidaktari hapa.

 

“Kwa mfano nikikuta mtu ana tatizo la uvimbe ninamfanyia oparesheni kwa kutumia vidole vyangu, hapa kila kidole kina kazi yake, vipo ambavyo ni maalum kwa kufanya upasuaji na vingine kwa ajili ya kushona,” alisema Nabii Nyakia.

 

VITANDA VYAJAA KANISANI

Ndani ya kanisa la nabii huyo siku ya oparesheni kunajaa vitanda maalumu ambavyo vinatumika kwa upasuaji na kwa mujibu wake ni kwamba anafanya hadharani watu wanaona.

“Kuna siku maalumu kwa ajili ya kufanya upasuaji ambapo waumini wote hushuhudia ninavyofanya, kuna mmoja alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa henia (ngiri) nikamfanyia upasuaji akapona kabisa,” alisema Nabii Nyakia.

 

MAREKANI WAMFUATA

Nabii Nyakia alisema kutokana na huduma hiyo kuwavutia, baadhi ya raia wa Marekani walimfuata na kumtaka akafanye nao kazi nchini mwao ambako angeenda na familia na watu wengine wa kumsaidia 11 na kwamba wangemlipa milioni 18 kwa mwezi lakini alikataa.

 

“Baada ya kukataa kwa mara ya kwanza maana bado nilikuwa sijasikia sauti ya Mungu kuhusiana na hilo, Wamarekani hao walirudi tena na kuniambia watanipa mshahara wa milioni 45 nikakataa pia maana namsikiliza Mungu zaidi, bado hajaniambia,” alisema Nabii Nyakia.

STORI: GLADNESS MALLYA, RISASI

 

Toa comment