MCHUNGAJI MATATANI KIFO CHA KIBONDE

MCHUNGAJI wa Kanisa la Emmaus Bible Church, Mbezi Luis jijini Dar, Daudi Mashimo amejikuta mikononi mwa poli­si baada ya kuzungumzia kifo cha mtangazaji wa Clouds FM, Ephraim Kibonde, Ijumaa Wikienda lina habari kamili.

 

NI IJUMAA ILIYOPITA

Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, mchungaji huyo ali­jikuta matatani Ijumaa iliyopita katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay ambapo alishikiliwa kuanzia majira ya saa 5 asub­uhi mpaka jioni alipoachiwa. “Aliwekwa pale kituoni kuan­zia mida kama ya saa tano hivi wakamuachia jioni sana baada ya kumuweka kitimoto cha maswali yao kuhusu Kibonde,” kilidai chanzo hicho.

 

KILICHOMPONZA

Mara baada ya kifo cha Kibonde kutokea Machi 7, mwaka huu, mchungaji Mashimo aliibuka na kutoa kauli kwamba mtangazaji huyo hajafa jambo ambalo liliwashangaza wengi ambao wanaamini kifo kikishatokea, kimetokea. “Kilichomponza ndio hicho, ameonekana kama anataka kusababisha vurugu kwa familia ambayo inaamini mpendwa wao ameshafariki,” kilieleza chanzo makini.

 

AANDAA PRESS

Kuonesha kwamba amed­hamiria kuzungumzia kinaga ubaga jambo hilo la Kibonde, mchungaji Mashimo aliona awatumie jumbe wanahabari kuonesha dhamira yake ya kufanya mkutano wa waandi­shi (press) ili aweze kufafanua kiundani. Press hiyo alipanga kuifanya Ijumaa iliyopita lakini badala yake, alitakiwa ajisalimishe kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano.

 

“Siku hiyohiyo ambayo ilikuwa afanye press, polisi walimuita ambapo walikaa naye kuanzia asubuhi mpaka jioni, kikubwa walikuwa wan­amhoji na kumuelekeza aache kuleta uchonganishi kutokana na kauli yake aliyoitoa kuhusu Kibonde kuwa yupo hai,” kili­malizia chanzo hicho makini.

HUYU HAPA MASHIMO

Baada ya kupewa ubuyu huo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta mchungaji Mashimo, Ijumaa iliyopita kupitia simu yake ya mkononi ambapo alipopa­tikana alithibitisha kushikiliwa na polisi na kueleza msimamo wake kuhusu suala hilo la Kibonde. “Unajua watu wanashindwa tu kunielewa kwamba si mimi bali ni Mungu mwenyewe anasema kupitia mimi. Nime­shaoneshwa mambo mengi huko nyuma nikayasema na kweli yakadhihirika mbona watu walikuwa hawashangai.

 

“Kwa hili la kifo nasima­mia msimamo wangu, yaani mpaka kesho huo ndio unabii wangu, mimi ni mtumishi wa Mungu nini kosa langu…ni maono hata kama wameni­piga marufuku siwezi kuacha kutoa unabii, nitaendelea kumsikiliza Mungu tu, haya ndio maisha yangu hivyo siwezi kuacha kuongea kile ambacho Mungu amenione­sha,” alisema mchungaji.

 

KAMANDA KINONDONI AFUNGUKA

Ijumaa Wikienda lilizungumza na Kamanda wa Kinondoni, Mussa Athumani Taibu am­baye alithibitisha kumhoji mchungaji Mashimo kwa saa kadhaa kabla ya kumuachia. “Tulimwita kwa shida zetu akidaiwa kusema kuwa Kibonde hajafa, wamezika mgomba anaweza kuleta uchonganishi kwa familia ikapelekea ramli chonganishi ambayo huleta maafa, hatu­jamzuia kufanya mikutano wala kuhubiri neno au ma­fundisho ya Mungu. Hicho tu ndicho tulichomwitia,” alisema kamanda Musa.

 

Kibonde alifariki baada ya kuugua ghafla mjini Bukoba alipokwenda kumzika ali­yekuwa bosi wake, Mkurugen­zi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba na kuzikwa Machi 9, mwaka huu katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar.

Stori: Mwandishi Wetu, Ijumaa Wikienda


Loading...

Toa comment